Mizengo Pinda, Waziri Mkuu mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametoa wito mzito kwa vyama vya ukombozi barani Afrika kuendeleza ushirikiano na mshikamano wao. Akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu Maalum wa vyama sita rafiki vya ukombozi Kusini mwa Afrika uliofanyika nchini Afrika Kusini, Pinda alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya ukombozi, misingi ya haki, na usawa katika maendeleo jumuishi. Lengo kuu ni kuhakikisha utekelezaji wa kweli wa Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo.
Katika hotuba yake kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM, Pinda alieleza kuwa vyama hivi rafiki – vikiwemo ANC (Afrika Kusini), MPLA (Angola), SWAPO (Namibia), ZANU PF (Zimbabwe), FRELIMO (Msumbiji), na CCM (Tanzania) – vina jukumu kubwa la kuhakikisha vinadumisha mshikamano. Alisisitiza kuwa misingi ya haki, usawa, na maendeleo shirikishi kwa wananchi wote ni ishara tosha ya kutekeleza kwa vitendo Ajenda 2063, kwa kuwa vyama hivi ndivyo vimebeba dhamana kubwa ya maendeleo barani humo.
Pinda alieleza kuwa mustakabali wa mataifa kama Tanzania, Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe, Angola, na Namibia unategemea sana uhusiano thabiti kati ya viongozi na wananchi wao. Aliwataka washiriki wa mkutano huo kutumia fursa hiyo kujenga fikra za vijana, kuwaelimisha kuhusu historia na misingi ya vyama vya ukombozi, na kuwajengea uzalendo. "Umuhimu wa kuwajumuisha vijana katika kila hatua ya harakati za kisiasa na maendeleo ya jamii ni njia muhimu ya kujenga kizazi cha vijana wazalendo," alisema Pinda. Aliongeza kuwa vijana wenye ufahamu wa kina kuhusu historia ya vyama hivi, kama ilivyokuwa kwa waasisi kama Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Nelson Mandela, na Sam Nujoma, ndio watakaoendeleza amani na maendeleo ya Afrika.
Alifafanua zaidi kuwa, endapo jamii itatambua mchango mkubwa wa waasisi hawa, basi maendeleo ya Afrika yatakuja kwa dhamira ya dhati ya kulinda, kudumisha, na kuendeleza misingi waliyoiweka. Hii itafanikiwa iwapo vijana watakuwa sehemu muhimu ya maendeleo hayo. Pinda alisisitiza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuwaunganisha viongozi na kuwataka wajenge mikakati ya kuendeleza mema yaliyoasisiwa na mababa wa taifa, huku wakiboresha vyama hivyo viendelee kuwa chachu ya mabadiliko kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mbali na kuhudhuria ufunguzi rasmi wa mkutano wa vyama rafiki vya ukombozi, Pinda pia alishiriki kikao maalum na ujumbe kutoka Chama cha Kikomunisti cha China (CPC). Katika kikao hicho, walijadili mikakati ya kimkakati kuhusu mwelekeo wa kisiasa na kijamii wa vyama vya ukombozi katika kizazi kipya cha uongozi barani Afrika. Mkutano huo, ulioanza Julai 25 na kuhitimishwa leo, ulikuwa na dhima kuu ya kutetea mafanikio ya ukombozi, kusukuma mbele maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi, na kuimarisha mshikamano kwa ajili ya Afrika yenye ustawi.