Kinyang'anyiro cha urais visiwani Zanzibar kinapamba moto, huku mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais anayetetea kiti chake, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akitarajiwa kuweka historia leo Septemba 6, 2025, kwa kuwa mgombea wa kwanza kurejesha fomu yake ya uteuzi katika ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Hatua hii ya Dk. Mwinyi inakuja ikiwa ni takriban wiki moja tu tangu alipochukua fomu hiyo Agosti 30, akionyesha dhamira thabiti ya kutetea nafasi yake katika uchaguzi mkuu unaosubiriwa kwa hamu mwezi Oktoba mwaka huu. Kitendo cha kuwa wa kwanza kurejesha fomu kati ya wagombea wote 17 waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo, kinatafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama ishara ya kujiamini na maandalizi thabiti ya chama chake kuelekea kampeni.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), zoezi la uchukuaji fomu lilianza rasmi Agosti 28 na litafikia tamati kwa urejeshaji wa fomu hizo mnamo Septemba 10. Baada ya hapo, Tume itafanya uhakiki na kutoa orodha rasmi ya wagombea watakaoshiriki uchaguzi huo.
Mara baada ya zoezi la urejeshaji fomu kukamilika, pazia la kampeni za uchaguzi linatarajiwa kufunguliwa rasmi Septemba 11, ambapo vyama na wagombea watapata fursa ya kunadi sera na ilani zao kwa wananchi wa Zanzibar. Wananchi wanasubiri kwa shauku kusikia ajenda za wagombea mbalimbali kabla ya kufanya maamuzi yao kwenye sanduku la kura.