Safari ya kampeni za Uchaguzi Mkuu imechukua sura ya kipekee na ya kitamaduni zaidi wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, baada ya Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, kurejea nyumbani kwao na kupokelewa kwa heshima nzito za kimila.
Tukio hilo la aina yake limetokea leo, Oktoba 19, Balozi Nchimbi alipowasili katika Kata ya Lituhi, Jimbo la Nyasa, akiwa katika mwendelezo wa mikutano yake ya kuomba kura kwa ajili ya Rais, Wabunge, na Madiwani. Hata hivyo, mapokezi yake hayakuwa ya shamrashamra za kawaida za kisiasa pekee, bali yalipambwa na matukio adhimu ya jadi yaliyoongozwa na wazee wa eneo hilo, yakilenga kumkaribisha rasmi na kumpa baraka zote za kuelekea katika uongozi wa juu wa kitaifa.
Shughuli nzima ya kimila ilisimamiwa na kiongozi mkuu wa jadi, Chifu wa Nyasa, Mheshimiwa Saad Wabu Musa, ambaye pia anashikilia wadhifa wa Katibu wa machifu wote wa Mkoa wa Ruvuma. Wazee hao walifanya taratibu kadhaa zenye uzito wa kipekee kuashiria kumtambua na kumbariki "mtoto wao aliyerudi nyumbani" akiwa katika jukumu jipya.
Katika matukio hayo yaliyofanyika mbele ya umati katika Uwanja wa Kata ya Lituhi, Balozi Dk. Nchimbi alishiriki kikamilifu. Awali, alizungushiwa unga safi wa mhogo, ikiwa ni ishara ya utakaso, kukubalika, na baraka kutoka kwa ardhi ya kwao. Kufuatia hilo, wazee hao walifanya tambiko la "kuita mizimu," wakiwasiliana na mababu zao kuwataarifu kwamba Dk. Nchimbi amerejea salama na anaomba ridhaa na nguvu zao katika safari anayoiendea.
Heshima haikuishia hapo. Dk. Nchimbi alivishwa rasmi vazi la jadi, shuka (linalojulikana kama mgolole), kabla ya kukabidhiwa zana za uongozi na mamlaka ya kimila: mkuki na ngao. Hii ni ishara ya kumvika mamlaka ya kulinda na kuongoza. Aidha, alikalishwa kwenye kigoda maalum (kiti cha jadi cha heshima) na kufungwa kitambaa chekundu kwenye paji la uso. Wazee walifafanua kuwa kitendo hiki cha mwisho kina maana kubwa, kwamba "ufalme sasa unatoka nyumbani na kuelekea serikalini," wakimpa baraka zote za ushindi.
Baada ya kupokea heshima hiyo kubwa na kutawazwa kuwa mmoja wa viongozi wa kimila, Balozi Dk. Nchimbi alitoa shukrani zake za dhati kwa wazee wa Nyasa. Alisema ameguswa na heshima hiyo na anaitambua kama deni kubwa kwake.
Aliwahakikishia wazee hao na wananchi wa Ruvuma kwa ujumla kwamba atafanya kila jitihada kuhakikisha anamsaidia kwa ufanisi mkubwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Alisisitiza kuwa atafanya kazi kwa bidii ili kumwamnisha Rais Samia asije akajutia uamuzi wake wa kumchagua mtu kutoka mkoani Ruvuma kuwa msaidizi wake. Dk. Nchimbi alikiri kwamba endapo atatoa msaada dhaifu kwa Rais, atakuwa amewaangusha vibaya wananchi wa Ruvuma na Ukanda mzima wa Kusini, na akaahidi kutowaangusha.