"Msikubali Kuwa Daraja la Vurugu" - Diwani Rajabu Atinga Kijiweni Didia, Afunguka Mazito kwa Bodaboda

politics | Sun Dec 14 2025


"Msikubali Kuwa Daraja la Vurugu" - Diwani Rajabu Atinga Kijiweni Didia, Afunguka Mazito kwa Bodaboda

Katika kile kinachoonekana kama ni hatua madhubuti ya kuimarisha ulinzi wa amani kuanzia ngazi ya shina, Diwani wa Kata ya Puni katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi Jumanne Rajabu, amefanya ziara ya kushtukiza na yenye tija katika kijiwe maarufu cha Njiapanda ya Didia kukutana na kundi muhimu la vijana wanaojishughulisha na usafirishaji wa abiria kwa pikipiki, maarufu kama Bodaboda.


Ziara hiyo iliyofanyika jana, haikuwa tu ya kisiasa bali ilibeba ujumbe mzito wa kiuchumi na kijamii. Mhandisi Rajabu, akizungumza kwa lugha ya kizalendo na yenye kuingia akilini, aliwapongeza vijana hao kwa ukomavu wao wa kisiasa na kuwataka waendelee kuwa mabalozi wa amani badala ya kukubali kutumiwa na wanasiasa uchwara au makundi yenye nia ovu ya kuvuruga utulivu wa Tanzania.


"Ndugu zangu vijana, ninyi ni nguvu kazi ya taifa hili. Amani ndiyo mtaji wenu mkuu. Ikitokea amani imetoweka leo, wa kwanza kuumia ni ninyi mnaotafuta riziki ya kutoa mkono kwenda kinywani," alisisitiza Mhandisi Rajabu huku akiwaasa vijana hao kutogeuzwa kuwa 'karai' la kujengea ajenda za vurugu.


Aliongeza kuwa, sekta ya bodaboda ni nyeti na inategemea sana mzunguko wa watu na usalama. Endapo nchi itaingia kwenye machafuko, hali hiyo itasababisha kile alichokiita "Lockdown" ya lazima, jambo ambalo litakata mrija wa mapato kwa vijana hao na familia zao zinazowategemea.


"Amani ya nchi ikichezewa, shughuli za maendeleo zitasimama nchi nzima. Ninyi mtashindwa kutoka barabarani kutafuta 'chenchi' ya kuendesha maisha na kuhudumia watoto wenu. Hivyo, nawasihi sana, kataeni kutumika kufanya maandamano yasiyo na tija wala afya kwa taifa letu," aliongeza kiongozi huyo.


Aidha, Mhandisi Rajabu hakusita kumtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kama kielelezo cha uongozi uliotukuka na wenye huruma, akiwataka vijana hao kumuunga mkono kwa vitendo kwa kulinda utulivu uliopo ili Rais aendelee kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi. "Tuna Rais mwenye upendo na uchu wa maendeleo, tumlinde kwa wivu mkubwa kwa kuhakikisha hatumpi nafasi yoyote mtu anayetaka kumkwamisha kwa kuvuruga amani," alisema.


Ujumbe huo ulipokelewa kwa mikono miwili na waendesha bodaboda hao. Wakiongozwa na kiongozi wao, Bw. Paul Laurent, vijana hao walisema wamejifunza kutokana na matukio ya hivi karibuni na hawako tayari tena kuwa wahanga wa siasa za majitaka.


Paul alibainisha kuwa, matukio ya taharuki yaliyotokea tarehe 29 Oktoba na siku ya Uhuru, Desemba 9, ambapo kulikuwa na shinikizo la watu kubaki majumbani, yaliwafunza somo chungu. "Siku zile tulipokaa ndani bila kazi, familia zetu zililala njaa. Sisi maisha yetu ni ya kutafuta leo tule leo. Hatupo tayari kurudia makosa hayo kwa ajili ya maslahi ya watu wachache," alisema Paul kwa uchungu.


Naye James Lugembe, mmoja wa waendesha bodaboda hao, alitumia nafasi hiyo kuliomba Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuongeza kasi ya kudhibiti viashiria vyote vya uvunjifu wa amani. Alisisitiza kuwa wananchi wanataka kufanya biashara zao kwa uhuru bila hofu ya kesho, huku akiamini kuwa serikali sikivu ya CCM itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kujikwamua kiuchumi.


Tukio hili katika Njiapanda ya Didia ni kielelezo tosha kuwa vijana wa Kitanzania sasa wameanza kuelewa thamani ya amani na uhusiano wake wa moja kwa moja na uchumi wao binafsi.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.