Hali ya simanzi na majonzi imetanda katika eneo la machimbo ya Nyandolwa, Wilayani Shinyanga, wiki mbili baada ya mgodi wa wachimbaji wadogo kuporomoka na kuwafunika watu 25, tukio ambalo limegusa taifa zima. Katika kuonesha uzito wa janga hili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameingilia kati kwa kumtuma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kufikisha salamu za pole na kutoa maagizo maalum kwa viongozi wa serikali.
Akizungumza kwa masikitiko katika eneo la tukio, Waziri Lukuvi alieleza kuwa Rais Samia ameguswa mno na msiba huu. Alisema amebeba ujumbe wa faraja na rambirambi kutoka kwa Rais kwenda kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao. Aidha, alitoa agizo la serikali, akisema, "Rais Samia amenituma kuleta maagizo kwa viongozi wote wa serikali hapa eneo la tukio. Ameagiza wahakikishe wanashiriki katika kila msiba, kuhudhuria mazishi yote na kuwakilisha rambirambi alizotoa kwa kila familia iliyoathirika."
Agizo hili linalenga kuhakikisha kuwa serikali inakuwa bega kwa bega na familia za wafiwa katika kipindi hiki kigumu. Akipokea maelekezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alihakikishia utekelezaji wake na kutoa taarifa ya hali inavyoendelea. Alibainisha kuwa miili ya marehemu inayoopolewa hupelekwa moja kwa moja katika chumba maalum cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga, Iselamagazi, na taratibu za kuwakabidhi kwa familia zimepangwa vizuri.
Wakati huo huo, zoezi la uokoaji linaendelea bila kuchoka, ingawa matumaini ya kupata manusura zaidi yanazidi kufifia. "Operesheni ya uokoaji inaendelea, na sasa tunatumia teknolojia ya kisasa, ikiwemo mashine maalum za kubaini maeneo ambayo huenda bado kuna miili, ili tuweze kuiopoa," alieleza Mboni.
Ajali hii ilitokea Agosti 11, 2025, na hadi sasa, ikiwa ni siku ya 14, watu 11 wamekwisha tolewa kutoka chini ya kifusi, ambapo watatu walipatikana wakiwa hai na wanane wakiwa wamefariki dunia. Bado kuna watu wengine 14 ambao hawajulikani walipo chini ya ardhi.