Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania imeendelea kusisitiza msimamo wake wa kutotambua Sekretarieti ya uongozi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayoongozwa na Katibu Mkuu wake, John Mnyika. Hatua hii inakuja baada ya sekretarieti hiyo kuteuliwa Januari 22 mwaka huu katika Baraza Kuu la chama hicho, kufuatia kupatikana kwa uongozi mpya chini ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Tundu Lissu.
Hii ni mara ya pili kwa Ofisi ya Msajili kutoitambua sekretarieti hiyo, ikidai kuwa akidi iliyotumika wakati wa uteuzi haikukidhi matakwa ya kikatiba na kikanuni ya chama hicho. Ofisi hiyo imeitaka CHADEMA kuitisha mkutano mwingine wa Baraza Kuu ili kuidhibitisha sekretarieti hiyo kwa kuzingatia sheria na kanuni za chama.
Malalamiko kuhusu kutotambuliwa kwa sekretarieti hiyo yaliwasilishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na mwanachama wa CHADEMA, Lembrus Mchome. Ofisi ya Msajili imetoa orodha ya majina ya wanachama ambao hawatambuliwi kama viongozi halali wa chama, ikiwa ni pamoja na John Mnyika, Amani Golugwa, Ali Ibrahimu Juma, Godbless Lema, Dk. Rugemeleza Nshala, Rose Mayemba, Salima Kasanzu, na Hafidhi Ali Saleh.
"Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inawasihi wananchi, wadau, mamlaka na taasisi zote za serikali na binafsi, kutowapa ushirikiano na huduma wanachama walioorodheshwa hapo juu, endapo watahitaji kuzipata kama viongozi wa CHADEMA," ilisema taarifa kutoka ofisi hiyo.
Ofisi ya Msajili imesisitiza kuwa CHADEMA inapaswa kufanya uamuzi wa busara kwa kuitisha kikao halali cha Baraza Kuu la Taifa na kujaza nafasi zilizo wazi, badala ya kupingana na sheria. "Vitendo vya kukaidi maagizo ya Msajili wa Vyama vya Siasa viliendelea kujitokeza," ilisema taarifa hiyo, ikirejelea kauli ya Makamu Mwenyekiti Bara wa CHADEMA aliyesema kuwa maamuzi ya Msajili ni batili.
Msajili wa Vyama vya Siasa amesikitishwa na msimamo wa CHADEMA na amesitisha utoaji wa ruzuku kwa chama hicho hadi watakapofuata maelekezo yake. "Kutokana na ombwe la uongozi wa chama hicho, Msajili wa Vyama vya Siasa ameamua kusitisha kuwapa ruzuku chama hicho hadi kitakapotekeleza maelekezo," ilisema taarifa hiyo.
Ofisi ya Msajili imekanusha madai ya CHADEMA kuwa imekuwa ikimsaidia Lembrus Mchome, na imesema kuwa malalamiko yake ni halali na yanafuata sheria. Ofisi hiyo pia imefafanua kuwa ina mamlaka ya kufanyia kazi malalamiko ya wanachama kuhusu ukiukwaji wa katiba na kanuni za vyama vya siasa.
Msajili amesema kuwa endapo CHADEMA itaendelea kukaidi maagizo yake, atazitaka mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanachama wanaojifanya viongozi. Pia, ana mamlaka ya kusimamisha usajili wa chama hicho.