Kauli mbiu ya kisiasa ya "No Reform, No Election" (Hakuna Marekebisho, Hakuna Uchaguzi) sasa imehamia rasmi visiwani Zanzibar, baada ya Mwenyekiti wa chama cha Alliance for Accountability and Forward Progress (AAFP), Said Soud, kutangaza msimamo mzito wa chama chake. Soud amesema bila kufanyika kwa mabadiliko ya kimsingi ndani ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), hakutakuwa na uchaguzi huru na wa haki, na kushiriki kutakuwa ni sawa na kumsindikiza tu rais aliyepo madarakani.
Akizungumza katika mahojiano maalum leo, Juni 10, 2025, Bw. Soud amethibitisha msimamo huo ambao ulikuwa umeanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa ni sharti lisilo na mjadala kwa upande wao.
"Ndio, msimamo wetu kwa upande wa Zanzibar ni 'No Reform, No Election'," alisema Soud. "Tunataka mabadiliko ya kweli katika muundo na utendaji wa Tume ya Uchaguzi. Bila marekebisho hayo, vyama vya siasa vitakuwa vinashiriki kwenye uchaguzi ili tu kukamilisha ratiba na kumsaidia Dk. Hussein Mwinyi kubaki madarakani. Hiyo sio demokrasia."
Alifafanua kuwa mabadiliko hayo ni muhimu ili kuweka uwanja sawa wa ushindani wa kisiasa na kuhakikisha matokeo ya uchaguzi yanaakisi kweli matakwa ya wananchi wa Zanzibar.
Wakati huo huo, akizungumzia hali ya ndani ya chama chake, Mwenyekiti huyo alikiri kuwepo kwa mgogoro na mvutano. Hata hivyo, alisema anaamini suluhu ya kudumu ya changamoto hizo za ndani ipo mikononi mwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye alimtaja kama "mlezi wa vyama vya siasa" nchini. "Hatuwezi kupata suluhu ya kudumu bila kumshirikisha msajili. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kusaidia kumaliza tofauti zetu," alihitimisha Soud.
Msimamo huu wa AAFP unaongeza sura mpya ya vuta nikuvute ya kisiasa visiwani Zanzibar kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.