Baada ya Mbunge wa Newala Mjini, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, kutangaza rasmi kuwa hatowania tena kiti cha ubunge, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeelezea hisia zake za shukrani na kutambua mchango wake mkubwa kwa taifa na jimbo la Newala.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, alitoa kauli yake leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Butiama, Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara. Akizungumzia uamuzi wa Mkuchika, Makalla alisema kuwa ni wachache sana wanaofikia hatua ya kustaafu na kuonyesha uungwana kwa kutangaza mapumziko yao.
"Mzee Mkuchika ameamua kupumzika, hivyo tunapaswa kumpata mtu mwenye nguvu na uwezo wa kuendeleza kazi aliyoifanya. Ni watu wachache sana wenye uungwana wa kuamua kupumzika wenyewe. Tunaahidi kuendelea kuchota busara zake na tunaamini atatoa ushirikiano wake," alisema Makalla.
Kwa upande wake, Kapteni Mkuchika aliwahakikishia wanachama wa CCM kuwa jimbo la Newala litaendelea kuwa ngome ya chama hicho. Alionya wapinzani wanaotarajia kuwania nafasi za ubunge na udiwani, akisema kuwa miaka mitano ijayo itakuwa ni ya ushirikiano kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na mbunge atakayechaguliwa, pamoja na madiwani.
"Ninashangaa kuona wapinzani wakitaka kuchukua fomu za ubunge na udiwani. Wanapaswa kujua kuwa Newala ni ya CCM," alisema Mkuchika. Aliwaonya wananchi wa Newala kuhusu kuchagua viongozi, akitumia mfano wa uyoga unaoliwa na usioliwa, akiwataka kuchagua viongozi sahihi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alimsifu Mkuchika kwa utumishi wake uliotukuka na kutaka atendewe haki kwa kazi nzuri aliyoifanya Newala. Alisema Mkuchika ni Mmakonde halisi ambaye amehudumu katika nafasi mbalimbali ndani ya CCM, jeshi, na serikali, na amekuwa waziri kwa zaidi ya miaka 17 bila kashfa.
"Mzee Mkuchika ni mfano wa kuigwa. Amefanya kazi kubwa na amestaafu akiwa msafi. Tunapaswa kumtakia kila la heri katika mapumziko yake," alisema Nape. Alisisitiza umuhimu wa kuwasemea mema watu wakiwa hai, akiongeza kuwa Mkuchika ameweka mfano mzuri kwa vijana kuhusu kuingia na kutoka madarakani kwa heshima.
"Wewe ni fahari yetu Kusini, umeitendea haki," alihitimisha Nape. Alionyesha imani kuwa Mkuchika hatafunga milango yake, na wataendelea kupata busara zake.