Majaliwa Apongeza Maandalizi ya Uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru Kibaha

politics | Sun Mar 30 2025


Majaliwa Apongeza Maandalizi ya Uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru Kibaha

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara ya siku moja katika uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha kukagua maendeleo ya maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa. Baada ya ukaguzi huo, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuridhishwa na kazi iliyofanyika, huku akitoa maelekezo ya kufanya maboresho zaidi katika baadhi ya maeneo ya uwanja huo kabla ya uzinduzi rasmi.


"Sina mashaka na maandalizi haya. Natarajia mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zitakuwa bora zaidi kuliko mwaka jana, na hii inatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi," alisema Waziri Mkuu Majaliwa.


Aliipongeza Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Kibaha kwa maandalizi makubwa waliyoyafanya, ambayo yamesababisha hata kusitisha baadhi ya shughuli zao za kawaida. Alisema maboresho yaliyofanyika katika uwanja huo yameufanya kuwa wa kiwango cha juu, kiasi kwamba unaweza kutumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


"Pia, kwa kuwa Tanzania imepata heshima ya kuandaa mashindano ya CHAN Afrika yatakayofanyika hapa nchini mwezi wa nane, na mahitaji ya viwanja ni mengi, tutakuja kukagua hapa. Ikiwa CAF (Shirikisho la Soka Afrika) wataridhika, watatupa kibali cha kuutumia uwanja huu," aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.


Aliwataka wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi wa mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kitaifa, ili kuungana na viongozi wa wilaya na kitaifa watakaohudhuria.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema maandalizi yanaendelea vizuri, ikiwa ni pamoja na kukamilisha maeneo yote ya uwanja. Alisema miundombinu imeboreshwa kwa kiwango kikubwa, na vijana wa halaiki wameandaliwa vizuri na wako tayari kushiriki katika tukio hilo la uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru.


Waziri Kikwete aliongeza kuwa wageni na wananchi zaidi ya 22,000 wanatarajiwa kushiriki katika uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, utakaofanyika Aprili 2 mwaka huu katika uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha. Uzinduzi huu ni tukio muhimu la kitaifa ambalo huadhimishwa kila mwaka na Watanzania.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.