Licha ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kufanikiwa kuvuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ametoa onyo kali kwa watumishi wa halmashauri hiyo, akiwataka kuziba mara moja mianya yote ya upotevu wa mapato.
Akizungumza katika kikao kazi na wakuu wa idara na vitengo wa Manispaa ya Shinyanga, RC Mhita alisema ingawa anawapongeza kwa kukusanya Shilingi bilioni 6.5 dhidi ya lengo la bilioni 6.4, hatavumilia kuona hata senti moja ya umma inapotea.
"Kila senti inayokusanywa lazima iingie kwenye akaunti ya serikali na isipotee. Fedha hizi zinahitajika kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kuendesha shughuli za Manispaa," alisisitiza Mhita.
Alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Alexius Kagunze, kuhakikisha anasimamia udhibiti wa mapato na wakati huohuo kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya manispaa.
Pamoja na suala la fedha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwakemea watumishi wasiowasikiliza na kuwahudumia wananchi kwa wakati, akisema ni jambo lisilokubalika. "Si jambo la busara kuona wananchi wanalalamika kuhusu huduma wakati ninyi mpo na mnalipwa mishahara. Ninyi mnapaswa kuwa suluhisho la kero zao, na si chanzo cha malalamiko," alisema.
Aidha, aliagiza miradi yote ya kimkakati ambayo bado haijakamilika ipewe kipaumbele na isimamiwe kwa umakini ili iwe na ubora unaotakiwa na kuleta manufaa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa, Mwalimu Kagunze, aliahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji ndani ya halmashauri yake.