Mgombea anayepeperusha bendera ya urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameingia jijini Dar es Salaam kwa kishindo, akizindua awamu mpya ya kampeni zake itakayodumu kwa siku kumi mfululizo. Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mbagala, ametuma salamu kali kwa washindani wake wa kisiasa, akidai kuwa upepo wa mabadiliko umeanza kuvuma na wale waliompuuza awali, sasa wameingiwa na hofu.
Akihutubia umati uliojitokeza, Mwalimu alieleza jinsi alivyodharauliwa na baadhi ya watu punde tu baada ya kuteuliwa kuwania wadhifa mkuu nchini. Hata hivyo, amesema kuwa baada ya kuzunguka katika mikoa 18 ndani ya siku 33 na kunadi sera zake, hali imebadilika kabisa. "Nilipoanza safari hii walinichukulia poa, lakini sasa sauti yangu na sera zangu zimewafikia Watanzania na zimeanza kuwatetemesha. Wameanza kukutana kwa vikao vya siri na mijadala imeongezeka, yote ni kwa sababu ya hofu," alisisitiza Mwalimu.
Aliongeza kuwa hatalegeza kamba na ataendelea kupambana usiku na mchana kuwafikia wananchi kila kona ya nchi hadi kieleweke. Dhamira yake kuu, kama alivyobainisha, ni kuleta mapinduzi ya kiuchumi yatakayomkomboa Mtanzania kutoka kwenye lindi la umaskini wa kipato.
Salum Mwalimu alitumia fursa hiyo kueleza kuwa chanzo cha maendeleo ya mataifa yaliyoendelea ni usimamizi thabiti na matumizi sahihi ya rasilimali zao. Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na mali asili nyingi, na iwapo itapata uongozi wenye uadilifu na uwajibikaji, ina uwezo kamili wa kufikia mafanikio makubwa ya kiuchumi na kuboresha maisha ya kila mwananchi.