Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, amewataka Watanzania kukipigia kura za kishindo chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao. Alisema kuwa yeye ametumwa kuwafikishia ujumbe kuwa mabadiliko makubwa yamefanyika nchini na hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuwazuia wananchi kwenda kupiga kura.
Alisisitiza kuwa maandalizi ya uchaguzi yanaanzia kwa wapiga kura kuhakikisha wana vitambulisho vya kupigia kura, na kuwataka wavitunze vizuri hadi wakati wa uchaguzi utakapofika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mei 22, 2025, huko Bariadi, mkoani Simiyu, wakati akiendelea na ziara yake ya siku saba, Makalla aliwahakikishia Watanzania kuwa CCM itawapelekea wagombea safi na wanaowajibika.
"Chama Cha Mapinduzi kimenituma kuwaeleza Watanzania kuwa mabadiliko makubwa yamefanyika. Msiwe na hofu yoyote, hakuna mtu mwenye ubavu wa kuwazuia kwenda kupiga kura. Tuendelee kuhubiri amani. Nimefurahi kusikia kauli ya Mkuu wa Mkoa kwamba, Simiyu itakuwa salama. Tutofautiane kwa itikadi, lakini tuiache Tanzania ikiendelea kuwa na amani," alisema Makalla.
Aliwaasa wananchi kutunza vitambulisho vyao vya kupigia kura akisema kuwa uchaguzi nchini hufanyika kila baada ya miaka mitano na ili chama kiweze kushika dola, lazima kishinde katika chaguzi zote kuanzia ngazi ya Serikali za Mitaa, udiwani, ubunge na urais.
"Uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi. Kila Mtanzania anajua kuwa kila baada ya miaka mitano, diwani, mbunge na Rais lazima wachaguliwe. Ndiyo maana mlikataa mikutano yao ya ‘No Reforms No Election’, haya maneno yao ni sawa sawa na ya kwenye kanga," alisisitiza Makalla.
Makalla alieleza kuwa uchaguzi hauwezi kuahirishwa au kucheleweshwa isipokuwa tu kama kutakuwa na vita.
"Ili kuonyesha kuwa Tanzania ina amani, walikuja hapa na kuomba mchango. Niwakumbushe Watanzania kuwa baada ya vita ya Kagera, tulitakiwa kufanya Uchaguzi Mkuu. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alishauriwa kuwa kutokana na vita, uchaguzi uahirishwe. Lakini alisema, 'chama changu kinaheshimu katiba, hivyo uchaguzi utafanyika'," alisema Makalla.
Aliwaambia wapinzani waliokuwa wamefanya mkutano wao huko Bariadi na kukosa wananchi, wasimlaumu Mkuu wa Mkoa kwani si kazi yake kuwaleta watu kwenye mikutano ya kisiasa.
"Wananchi wamejenga imani kwa CCM kwa sababu wanaona huduma za kijamii zilizofanywa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Mtu hajawahi kulima pamba anatoka Arusha anakuja Simiyu anasema nyie ni maskini. Wana-Simiyu si maskini, ni wachapakazi. Rais Samia ameweka alama kila kijiji, kila kata kuna huduma za kijamii za elimu, afya na barabara," alisisitiza Makalla.