Hali ya hewa imechafuka katika Kata ya Viziwaziwa, Manispaa ya Kibaha, baada ya Meya wa Manispaa hiyo, Dk. Mawazo Nicas, kushindwa kuzuia hasira zake dhidi ya watendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (DAWASA). Katika ziara yake ya kikazi iliyolenga kusikiliza kero za wananchi hapo jana, Desemba 23, 2025, Meya Nicas amejikuta akizungumza kwa uchungu baada ya Mhandisi wa mamlaka hiyo kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu ukame wa muda mrefu unaoikabili kata hiyo.
Meya Nicas, ambaye alikuwa ameambatana na wataalamu mbalimbali wa Manispaa, alipokelewa na 'mvua' ya malalamiko kutoka kwa wakazi wa Viziwaziwa. Kilio kikubwa cha wananchi kilikuwa ni kitendo cha kuunganishiwa miundombinu ya maji ambayo imebaki kuwa mapambo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Hali hiyo imetafsiriwa kama dhihaka kwa jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za "kumtua mama ndoo kichwani."
Mmoja wa wananchi wenye hasira, Hassan Omari, alieleza masikitiko yake mbele ya hadhara hiyo akidai kuwa, licha ya bomba lake kutotoa hata tone la maji, amekuwa akipokea ujumbe wa simu (SMS) ukimtaka alipe bili za maji ambayo hajayatumia. "Huu ni unyanyasaji! Maji hayatoki, mita wameiondoa, lakini bili zinakuja kama kawaida. Tunalipia hewa?" alihoji Omari huku akishangiwa na wenzake kama Venansia Ndunguru na Liberata Remi ambao pia waligusia kutaabika kwao kutokana na ukosefu wa huduma hiyo muhimu.
Kutokana na kigugumizi cha watendaji wa DAWASA kutoa suluhisho la haraka, Meya Nicas ametoa pendekezo zito kwa Waziri wa Maji. Ameomba Serikali ifikirie kuwarejesha watumishi wa DAWASA chini ya usimamizi wa Mamlaka za Halmashauri (LGAs). Alisisitiza kuwa muundo wa sasa unawapa watumishi hao mwanya wa 'kujiumauma' na kukwepa kutoa majibu ya moja kwa moja kwa viongozi wa wananchi.
"Wakati sisi viongozi tunakesha kuhakikisha ahadi za Rais za siku 100 na utekelezaji wa Ilani ya CCM unakwenda sawia, wenzetu wa DAWASA wanaonekana kutuangusha. Ikiwezekana, warudi Halmashauri tuwanyooshe huku," alisema Dk. Nicas kwa msisitizo.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Kituo cha DAWASA Kibaha, Eleminata Matindu, alijitetea kwa kusema kuwa mchakato wa kuleta maji Viziwaziwa upo mbioni. Alidai kuwa upembuzi yakinifu umeshakamilika na mradi unatarajiwa kuanza kutoa matunda ndani ya miezi mitano ijayo. Hata hivyo, kauli hiyo ilionekana kutowapoza wananchi ambao tayari wameshasikia ahadi nyingi zisizotekelezeka.
Kibaha, ikiwa ni kitovu cha viwanda na makazi yanayokua kwa kasi mkoani Pwani, inategemea sana huduma ya maji ili kuchochea uchumi wake. Kukosekana kwa huduma hii kwa ufanisi kunaathiri siyo tu afya ya jamii, bali pia kasi ya uwekezaji katika ukanda huo wa viwanda.