Meneja wa Kampeni wa chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa, ameibua tuhuma nzito za ubadhirifu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Tomondo, Zanzibar. Mbele ya maelfu ya wananchi, Jussa alidai kuwa kuna wizi wa wazi unaofanywa katika miradi ya ujenzi ya serikali.
Akifafanua, Jussa alitoa mfano wa bei ya saruji, akisema, "Hii ni aibu na dhulma ya wazi. Wakati mfuko wa saruji sokoni unauzwa Shilingi 17,000, wao kwenye hesabu za miradi wanaweka Shilingi 23,000. Hii tofauti ya Shilingi 6,000 kwa kila mfuko ni wizi unaofanyika Unguja na Pemba na kuwaumiza wananchi." Madai hayo yalipokelewa kwa shangwe na kelele na umati uliofurika kumsikiliza.
Jussa hakuishia hapo, alienda mbali zaidi na kuvituhumu vikosi vya ulinzi na usalama vya Zanzibar (SMZ) kuwa vinatumiwa vibaya kwa maslahi ya wachache. Alidai kuwa vikosi hivyo vimegeuzwa kuwa "walinzi wa makampuni binafsi" kutoka Dar es Salaam, na askari kulazimishwa kufanya kazi zisizo za kwao ili kulinda maslahi ya watu binafsi, jambo aliloliita dharau kwa taasisi hiyo muhimu na kwa wananchi wote.
Kwa upande wake, Mgombea Urais wa chama hicho, Othman Masoud Othman, alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa serikali yake itakomesha vitendo hivyo. Aliahidi kuwa, endapo atachaguliwa, atahakikisha mali za umma zinalindwa kwa gharama zote na heshima ya vikosi vya SMZ inarejeshwa.
"Serikali ya ACT Wazalendo itahakikisha miradi yote ya maendeleo inawanufaisha Wazanzibari moja kwa moja, na si kuwa chanzo cha wizi na ubadhirifu. Tutarejesha nidhamu na uwajibikaji serikalini," aliahidi Othman, huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.