Katika hatua ya kimkakati ya kuimarisha usimamizi na ulinzi wa maslahi ya wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza program maalum ya kuwanoa Mawakili wa Serikali. Akifungua mafunzo hayo maalum, Mwanasheria Mkuu, Mhe. Hamza Johari, amewataka mawakili hao kutumia maarifa watakayopata kama ngao ya kisheria kuhakikisha haki za wanachama wa mfuko huo zinalindwa ipasavyo.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yaliyoandaliwa na kufadhiliwa na PSSSF na kufanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere mkoani Pwani, yanalenga kuwajengea Mawakili wa Serikali uwezo wa kina kuhusu sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya hifadhi ya jamii. Mhe. Johari alisisitiza kuwa uelewa wa kina wa Sheria ya PSSSF, Sheria ya Mikataba, na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ni nyenzo muhimu itakayowawezesha kutoa ushauri sahihi na thabiti.
"Matarajio yangu ni kwamba mafunzo haya yatawapa weledi wa kutosha sio tu katika muundo wa PSSSF, bali pia katika haki na wajibu wa wanachama, wastaafu na wategemezi wao," alisema Mhe. Johari. Aliongeza kuwa serikali inataka kuona Mawakili wake wanakuwa chanzo cha kupunguza migogoro ya kisheria inayohusu mfuko huo, kwa kutumia mbinu za usuluhishi badala ya kusubiri kesi kufika mahakamani, jambo litakalookoa muda na rasilimali za serikali.
Mwanasheria Mkuu alieleza kuwa ushirikiano huu wa karibu kati ya Ofisi yake na PSSSF ni muhimu kwa maslahi mapana ya Taifa. Aliwasihi washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha maarifa wanayopata hayabaki darasani, bali yanakwenda kubadilisha utendaji kazi wao wa kila siku na kuhakikisha PSSSF inaendeshwa kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa kuzingatia sheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PSSSF, Vupe Ligate, alibainisha kuwa lengo kuu la kuendesha mafunzo hayo ni kurahisisha kazi ya Mawakili wa Serikali wanapohitaji kutoa ushauri wa kisheria kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii, na hivyo kujenga uelewa wa pamoja utakaoharakisha utoaji wa haki.