Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ADC (Alliance for Democratic Change), Hamad Rashid Mohammed, ametoa msimamo thabiti wa chama chake kuhusu Muungano, akiahidi kuuimarisha na kuudumisha, huku akionya dhidi ya wanasiasa wanaotoa kauli za kuupuuza au kuuvunja.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika viwanja vya Mwenge, Makunduchi mkoani Kusini Unguja, Hamad Rashid alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa nguzo ya mshikamano na mfano wa kuigwa kimataifa, na hakuna chama makini cha siasa kinachoweza kubeza thamani yake.
"Chama chochote makini hakiwezi kubeza Muungano. Huu ndio umetuunganisha na kutufanya kitu kimoja, na leo ni mfano unaoheshimika hata kwa mataifa ya nje," alisema mgombea huyo.
Alisisitiza kuwa amani na mshikamano uliopo nchini unatokana na kuwepo kwa Muungano. Kwa sababu hiyo, aliwataka wananchi wa Zanzibar kupima kwa makini kauli zote zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kuhusu madai ya kuvunja Muungano, akisema kauli hizo ni za hatari kwa umoja wa taifa.
Hamad Rashid alihitimisha kwa kusema kuwa ADC iko tayari kulinda Muungano kwa nguvu zote, akiongeza: "Hatuwezi kuruhusu uvunjike, tutaendelea kuusimamia na kuudumisha," kwani Muungano umelipa heshima kubwa taifa la Tanzania.