Katika hali ya kuonyesha uzalendo uliotukuka na uongozi wa vitendo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameongoza mamia ya wakazi wa mkoa huo katika zoezi maalum la usafi wa mazingira, huku akitumia jukwaa hilo kutoa ujumbe mzito wa 'Onyo na Nasaha' kuhusu mustakabali wa amani ya Tanzania.
Tukio hilo lililofanyika jana katika Manispaa ya Singida, lililenga kuadhimisha Miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania Bara (Tanganyika), siku ambayo ina uzito wa kipekee katika historia ya Taifa. Hata hivyo, tofauti na hotuba za kawaida za jukwaani, RC Dendego alichagua kuingia mtaani, akishikiana na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri, na watumishi wa umma kuchafua mikono ili kuuweka mji safi, ishara ya utayari wa kuijenga nchi kwa vitendo.
Akizungumza kwa hisia kali katika eneo la Ginery baada ya kuhitimisha zoezi hilo lililohusisha usafi wa masoko, mifereji, na barabara kuu, Dendego alisisitiza kuwa usafi wa mazingira unapaswa kwenda sambamba na usafi wa mioyo na fikra za Watanzania katika kulinda tunu ya amani.
Singida Yagoma Kuyumbishwa
Katika kile kilichoonekana kama pongezi za dhati kwa wananchi wake, Mkuu huyo wa Mkoa aliwamwagia sifa wakazi wa Singida, hususan vijana, kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa na kutokubali kutumika katika vurugu zilizoripotiwa maeneo mengine mnamo Oktoba 29 mwaka huu.
"Singida mmethibitisha kuwa ninyi ni waungwana. Licha ya changamoto zilizopo, ambazo ni jambo la kawaida katika jamii yoyote, mlichagua njia ya ustaarabu. Mlipeleka hoja zenu mezani badala ya barabarani," alisema Dendego na kuongeza:
"Amani yetu ndio mtaji wetu mkubwa. Hapa Singida, amani ndio msingi wa uchumi wetu. Nawashukuru sana vijana kwa kukataa kuwa chambo cha vurugu. Huu ndio uzalendo tunaoutaka."
Onyo Kali kwa 'Wapiga Debe' wa Ughaibuni
Dendego hakumung'unya maneno alipoelekeza kombora lake kwa watu wanaodaiwa kuchochea vurugu nchini wakiwa wamejificha nchi za nje. Alibainisha kuwa ni upumbavu kwa kijana wa Kitanzania kudanganyika na mtu ambaye "anakula maisha" ughaibuni huku akitaka damu imwagike nyumbani.
"Wanaowachochea mkaandamane, mchome ofisi na kuharibu miundombinu, wengi wao hata hawapo hapa nchini. Wapo huko wanakunywa mvinyo na familia zao, wanataka ninyi mharibu maisha yenu. Tuwapuuze na kuwaona kama maadui namba moja wa ustawi wa Singida na Tanzania kwa ujumla," alisisitiza kiongozi huyo.
Alikumbusha kuwa madhara ya kuvurugika kwa amani hayachagui chama wala kabila, na waathirika wakubwa siku zote ni wanawake, watoto, na wenye ulemavu. Alitolea mfano wa mataifa jirani ambayo yameingia kwenye machafuko na mpaka sasa yanahangaika kurejesha utulivu, jambo ambalo Tanzania haipaswi kuliiga.
Tanzania ni Nyumba Moja
Akigusia dhana ya Umoja wa Kitaifa, Dendego alitumia mfano hai wa maisha ya Kitanzania ambapo mwingiliano wa makabila na dini umeifanya nchi kuwa kama familia moja kubwa isiyoweza kutenganishwa.
"Hivi leo utatugawaje? Ingia kwenye nyumba nyingi Singida, unakuta Baba ni Mnyiramba, Mama ni Mchaga. Au Baba ni Muislamu, Mama ni Mkristo, na wanaishi kwa upendo. Sisi tumeunganishwa na damu na historia, siasa zisizotutakia mema zisipewe nafasi. Asikudanganye mtu, hayupo mama mwingine duniani kama Tanzania," alihitimisha kwa kauli hiyo iliyoibua hamasa kubwa.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Singida, Geofrey Mdama, alieleza kuwa Manispaa hiyo imejipanga kuhakikisha usafi unakuwa endelevu na sio wa matukio pekee. Aliahidi kusimamia sheria ndogo za jiji kikamilifu ili kuhakikisha Singida inabaki kuwa kioo cha usafi na mpangilio mzuri katikati ya Tanzania.
Maadhimisho haya ya Miaka 64 ya Uhuru yameacha alama Singida, si tu kwa mji kung'aa, bali kwa ujumbe mzito uliopandikizwa ndani ya mioyo ya wananchi kuhusu wajibu wao wa kulinda 'Nyumba Tanzania'.