Katika kile kinachoonekana kama kunoa makali ya safu ya uongozi ili kuendana na kasi ya Awamu ya Sita, Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mhe. Frank Nkinda, amewasha moto kwa Madiwani wa Manispaa hiyo, akiwataka kutumia dhamana waliyopewa kuacha urithi uliotukuka badala ya kuwa viongozi wa kusindikiza namba.
Rai hiyo nzito ameitoa leo wakati akifungua rasmi semina elekezi (Induction Course) iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya Madiwani hao. Mafunzo hayo, ambayo ni kama ‘kufua upya injini’ za viongozi hao wa kisiasa, yanatolewa na wobezi wabobezi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo) kilichopo jijini Dodoma.
Akizungumza kwa lugha ya picha na yenye kujaa hamasa za kizalendo, DC Nkinda amesema wakati wa "kucheka na nyani" shambani umekwisha. Amewakumbusha madiwani hao kuwa kura walizopigiwa na wananchi sio tiketi ya starehe, bali ni deni linalolipika kwa sarafu moja tu: Maendeleo yanayoonekana kwa macho.
"Waheshimiwa Madiwani, uongozi ni alama. Msiwe viongozi wa kupita kama upepo. Wananchi wa Kahama wanataka kuona mabadiliko, wanataka kuona kero za maji, barabara na afya zinatatuliwa. Hatuwezi kuwa na viongozi mnaolala usingizi wakati wananchi wenu wana shida. Lazima mkasimamie miradi hii kuanzia hatua ya michoro kwenye karatasi hadi inapokamilika na kuanza kutoa huduma," alisisitiza Nkinda huku akishangiliwa.
Kahama, ambayo inasifika kama kitovu cha biashara na uchumi katika Kanda ya Ziwa kutokana na shughuli za madini na kilimo, inahitaji usimamizi madhubuti wa rasilimali. Nkinda aliongeza kuwa jicho la diwani linapaswa kuwa kali katika kuangalia fedha za miradi ili kuhakikisha hakuna "panya" wanaotafuna jasho la walipa kodi. Aliwataka kujenga daraja la mawasiliano ya karibu na wataalamu wa Halmashauri pamoja na viongozi wa vijiji na mitaa ili kuondoa urasimu usio wa lazima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Ndugu Masudi Kibetu, amebainisha kuwa mafunzo hayo yamekuja muda muafaka. Amesema kwa kuwa Baraza la Madiwani lina sura mpya nyingi, semina hiyo itafanya kazi kama dira ya kuwaepusha na migongano ya kimajukumu (conflict of interest) kati ya wanasiasa na wataalamu.
"Tunataka kuona madiwani wetu wanajua mipaka yao na wajibu wao. Hii itasaidia sana katika kuongeza ufanisi wa kukusanya mapato ya ndani. Tunapokusanya vizuri, ndipo tunapopata fedha za kurudisha kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo, na hili linawezekana tu kukiwa na maelewano na uelewa wa pamoja," alisema Kibetu.
Naye Ofisa Tawala Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Bw. Mashaka Makuka, amefafanua kuwa mtaala wa mafunzo hayo umesheheni mada nyeti zinazogusa uti wa mgongo wa utawala bora. Ametaja kuwa madiwani hao watapikwa katika maeneo ya Sheria za Serikali za Mitaa, Uendeshaji wa Vikao (Standing Orders), Mipango na Bajeti, Usimamizi wa Ardhi na Watumishi, pamoja na Udhibiti wa Fedha.
Mafunzo haya yanatazamiwa kuleta mapinduzi makubwa katika utendaji wa Manispaa ya Kahama, huku wananchi wakiwa na matumaini makubwa kuwa "shule" watakayoipata viongozi wao itatafsiriwa kwa vitendo katika kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa wilaya hiyo.