Kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Mheshimiwa Olivanus Thomas, ametoa maagizo mazito yanayolenga kukomesha vitendo vya uharibifu wa vyanzo vya maji na wizi wa huduma hiyo muhimu. Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Iwela mnamo Oktoba 9, 2025, Mkuu huyo wa Wilaya aliagiza uongozi wa kata na kijiji kuwachukulia hatua kali, ikiwemo kuwakamata na kuwatoza faini, wafugaji wote watakaobainika kuingiza mifugo yao kwenye maeneo ya vyanzo vya maji.
Agizo hilo la papo kwa papo linatokana na kero iliyowasilishwa na wananchi kuhusu jinsi mifugo inavyochangia kuharibu na kuchafua vyanzo hivyo, jambo ambalo linahatarisha upatikanaji wa maji safi na salama. "Tuna sheria ndogo za halmashauri zinazolinda rasilimali zetu. Hatuwezi kuendelea kufumbia macho uharibifu huu ukiendelea. Nataka hatua zianze kuchukuliwa mara moja bila kumuonea mtu aibu," alisisitiza Thomas.
Katika muktadha huo huo, Mkuu wa Wilaya aliwageukia wataalamu kutoka Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), akiwaagiza kuanzisha msako mkali dhidi ya watu wote wanaojiunganishia huduma ya maji kinyemela. Alisema kitendo hicho cha wizi sio tu kinakiuka sheria, bali pia kinasababisha usumbufu na upungufu wa maji kwa wananchi wengine wanaofuata taratibu na kulipia huduma hiyo.
Mheshimiwa Thomas yupo kwenye ziara ya kikazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wilayani humo, akiwa ameambatana na timu nzima ya wataalamu ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Sunday Deogratias. Timu hiyo imefanya mikutano katika vijiji vya Nsungu, Mbongo na kata ya Iwela, ikilenga kuleta suluhu za haraka kwa changamoto zinazowakabili wananchi.
Sambamba na kusikiliza kero, Mkuu huyo wa Wilaya pia anakagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Alitembelea na kukagua ujenzi wa Barabara ya Nsungu–Ilela, Zahanati ya Mbongo, na Shule ya Sekondari ya Kata ya Iwela, ambapo aliwataka wakandarasi na wasimamizi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa kasi na ubora unaotakiwa ili ianze kuhudumia jamii kama ilivyokusudiwa.