Hatimaye kilio cha mwalimu mstaafu, Zacharia Basso, wa Babati kimesikika baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Emmanuela Kaganda, kuingilia kati na kuagiza Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Mji kuhakikisha anarejeshewa haki yake ya umiliki wa viwanja 15. Hatua hiyo ya kiongozi huyo imekuja kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya mwalimu huyo aliyedai kunyimwa haki yake na baadhi ya maafisa huku wengine wakivamia na kujenga kwenye maeneo yake kinyume cha sheria.
Akizungumza kwa uchungu mbele ya Mkuu wa Wilaya wakati wa mkutano wa kusikiliza kero za wananchi, Mwalimu Basso alieleza kuwa kati ya viwanja 76 alivyokuwa akimiliki, Halmashauri ilitakiwa kumpa fidia ya viwanja 15, jambo ambalo halikutekelezwa. Badala yake, alidai kuwa watu wasiojulikana walivamia na kujenga kwenye viwanja vyake nane na hata kufikia hatua ya kumtishia maisha alipojaribu kufuatilia haki yake.
Kufuatia maelezo hayo, DC Kaganda alionyesha kukerwa na kitendo hicho na akatoa maagizo thabiti kwa idara ya ardhi. "Haki ya mnyonge haiwezi kudhulumiwa hivi. Nataka wale waliojenga kwenye viwanja vinne waletwe mara moja na wamlipe fidia stahiki mzee huyu, na pia alipwe fidia kwa viwanja vingine 11 vilivyosalia," aliagiza Kaganda.
Aidha, aliamuru kufanyike kikao cha pamoja kitakachomshirikisha mwalimu huyo mstaafu, maafisa ardhi, na wale wote walionunua au kujenga kwenye maeneo hayo ili suala la fidia likamilishwe kwa uwazi. Alisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekaidi agizo la kulipa fidia hiyo.
Kwa upande wake, Mwalimu Basso alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa msimamo wake imara na kwa kumsikiliza, akieleza kuwa ana imani kuwa hatimaye haki itatendeka baada ya miaka mingi ya kuteseka na kufuatilia bila mafanikio.