Kapteni Mstaafu John Chiligati, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mnenaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, amewamwagia sifa kemkem mawaziri wenzake wa zamani, Ezekiel Maige na William Ngeleja. Chiligati amewataja wawili hao kama mifano bora ya wanasiasa wachapakazi, waadilifu, na wenye weledi wa hali ya juu, akisisitiza kuwa wanapaswa kuigwa na kizazi cha sasa cha wanasiasa vijana.
Kauli hizo za pongezi zilitolewa na Kapteni Chiligati alipokuwa akitoa salamu zake za rambirambi kwenye msiba wa baba yake Ngeleja, Mzee Mganga Ngeleja Nyashishi, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96 (1929-2025). Mazishi hayo yalifanyika Julai 21, mwaka huu, nyumbani kwa marehemu, kijiji cha Bitoto, wilayani Sengerema. Chiligati alitumia fursa hiyo kueleza jinsi alivyowafahamu Maige na Ngeleja tangu mwaka 2005 walipoingia bungeni, akiwatambua kuwa vijana wenye uwezo mkubwa wa kiuongozi na weledi licha ya umri wao mdogo kisiasa.
Kwa mujibu wa Kapteni Chiligati, Maige aliitumikia kwa ufanisi mkubwa Wizara ya Maliasili na Utalii, huku Ngeleja akitambulika kwa utendaji wake bora katika Wizara ya Nishati na Madini, aliyoiongoza kuanzia mwaka 2007 hadi 2012. Chiligati aliwafafanua wanasiasa hao kuwa walikuwa hodari, wachapakazi, na makini, na kwamba walikuwa tegemeo na kipenzi cha Rais Mstaafu Kikwete ndani ya Baraza lake la Mawaziri.
Akielezea siri ya Rais Kikwete kuwaibua wanasiasa hao, Kapteni Chiligati alisema ilitokana na uwezo wao wa kipekee katika kujenga hoja bungeni na kuuliza maswali yenye maslahi mapana kwa taifa na majimbo yao. "Kikwete, kama wengine mnavyofahamu, tulikuwa watu wa karibu sana, kwani tulifahamiana toka tunasoma sekondari na baadaye kufanya kazi pamoja kwa muda mrefu ndani ya CCM, jeshini na serikalini," alianza kueleza Chiligati. Aliendelea kufafanua kuwa, "Siku moja Kikwete alinieleza kuhusu hawa vijana Ngeleja na Maige, kuwa anawafurahia sana na kwamba wako ‘intelligent na smart’, akaniuliza mimi ninawaonaje? Nikamjibu, kwa kweli ni hodari na weledi zaidi. Baada ya mazungumzo hayo, sikujua Rais Kikwete alikuwa anapanga nini juu yao. Baada ya miezi michache, akatangaza kuwateua kuwa manaibu Waziri. Tulidumu nao kwenye Baraza la Mawaziri, tangu wakiwa manaibu waziri na baadaye kuwa mawaziri kamili. Hakika walikuwa vijana hodari, wabunifu na wachapakazi."
Kutokana na upendo na ukaribu aliokuwa nao na Ngeleja, Kapteni Chiligati alisema alihisi wajibu wa kuhudhuria mazishi ya baba yake, akimtaja Ngeleja kama "mdogo wake wa kumlea kisiasa" tangu walipokuwa bungeni. Akizungumzia uchaguzi ujao, Kapteni Chiligati aliwashauri wananchi kuchagua viongozi wenye uwezo na kusema kuwa CCM inahitaji vijana wanaokijua vizuri chama, wenye uwezo, na wazalendo kwa nchi yao ili kuharakisha maendeleo, akiwataja Ngeleja na Maige kama mifano halisi.
William Ngeleja alimshukuru Kapteni Chiligati na waombolezaji wengine kwa kufika kumfariji na kutambua mchango wake na wa marehemu baba yake kwa jamii na taifa. Mzee Nyashishi alifariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya Bugando, ambako alikuwa akipatiwa matibabu. Viongozi wengine mashuhuri waliohudhuria msiba huo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, na Ezekiel Maige mwenyewe.