Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeeleza kuwa kinafuatilia kwa umakini mkubwa tuhuma zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu madai ya kupigwa kwa Sigrada Mligo, Mratibu wa Uenezi wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa chama hicho.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, chama hicho kimesema kinafanya uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali ndani na nje ya chama, ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
"Tunafuatilia kila hatua inayochukuliwa, na tutatoa taarifa rasmi kuhusu suala hili kadri itakavyofaa," alisema Rupia katika taarifa hiyo.
Mbali na kufuatilia madai hayo, Chadema pia kimemwonya kiongozi huyo wa uenezi kuwa makini na uhusiano wake na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kuepuka kutumiwa kwa malengo ambayo yanaweza kuathiri hadhi ya chama na usalama wake binafsi.
Madai yanaeleza kuwa Sigrada Mligo alipigwa Machi 25 mwaka huu mkoani Njombe, na mmoja wa walinzi wa Chadema wakati wa kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche.
Tukio hili limezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii, huku wadau mbalimbali wakitoa maoni tofauti kuhusu madai hayo. Chadema imeahidi kutoa taarifa zaidi baada ya uchunguzi kukamilika.