Kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam wa takriban wiki moja iliyopita, uliokizuia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanya shughuli za kisiasa, chama hicho sasa kimegeukia katika shughuli za kijamii ili kuendeleza kampeni yake ya ‘No Reforms No Election’. Lengo kuu ni kuendelea kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini.
John Heche, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Bara), ametoa maelekezo kwa viongozi wote wa chama nchi nzima kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii. Shughuli hizi ni pamoja na kupanda miti, kutembelea wagonjwa hospitalini, na kutembelea watoto yatima. Hatua hii inalenga kuendeleza juhudi za chama katika kupigania uchaguzi huru na wa haki, huku kikijiepusha kutumia rasilimali za chama kwa shughuli za kisiasa kama ilivyoelekezwa na Mahakama.
Heche alisisitiza kuwa lengo la kampeni yao ni kuhakikisha kura ya mwananchi inakuwa na nguvu, ili serikali iweze kuwajibika kwa wananchi ipasavyo, kama inavyoelekezwa na Katiba ya nchi. "Sisi tunataka kura iwe na nguvu ili Serikali iwajibike kwa wananchi, wananchi ndio wawe na uwezo wa kusema kama Katiba inavyosema, ndiyo tunachojaribu kusema wananchi waelewe ili watuunge mkono," alifafanua Heche. Alihoji pia utayari wa baadhi ya viongozi kujitolea kwa ajili ya wananchi. "Kuna watu wanasema watapoteza ndoto zao za kuwa wabunge, kuwa madiwani; sasa watu kama hao wananchi watawapiganiaje mpaka kufa kama wao hawana uwezo wa kukubali kupoteza ubunge, udiwani au hata Urais kwa ajili ya kupigania wananchi?" alisema Heche, akihimiza kujitolea kwa viongozi.
Uamuzi wa Mahakama wa kusitisha shughuli za kisiasa za CHADEMA ulitokana na hati ya malalamiko iliyowasilishwa, ambapo walalamikaji wanadai kuwepo kwa mgawanyo usio sawa wa rasilimali za kifedha kati ya Bara na Zanzibar ndani ya chama hicho. Malalamiko mengine yaliyotajwa ni pamoja na madai ya ubaguzi wa kijinsia, udini, na matamko yanayodaiwa kuwa na nia ya kuvuruga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Uamuzi huu wa Mahakama ulitolewa baada ya Wakili wa CHADEMA, Jebra Kambole, kujiondoa katika kuendelea kuisimamia kesi hiyo mapema Jumanne. Kambole alilalamika kuwa hoja za mawakili wao hazikusikilizwa ipasavyo, jambo lililopelekea uamuzi wake wa kujiondoa. Hali hii inaendelea kuweka siasa za Tanzania katika taharuki, huku wananchi wakisubiri kuona ni kwa jinsi gani CHADEMA itaendeleza malengo yake kupitia mikakati mipya ya kijamii.