Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ameweka wazi mipango kabambe ya chama hicho inayolenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi katika Mkoa wa Singida ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo. Akizungumza na umati wa wananchi katika eneo la Puma, Dk. Nchimbi alifafanua kuwa serikali ijayo itawekeza nguvu kubwa katika sekta za kilimo, ufugaji, na madini ili kuinua maisha ya wananchi wa mkoa huo.
Katika sekta ya kilimo na ufugaji, ambayo ni uti wa mgongo wa wakazi wengi wa Singida, Dk. Nchimbi aliahidi kuwa serikali itajenga miundombinu muhimu itakayobadilisha kabisa sura ya uzalishaji. Alisema kuwa mpango mahususi upo wa kujenga majosho kwa ajili ya mifugo pamoja na malambo ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhi maji ya mvua, hatua itakayokuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima na wafugaji wanaotegemea kilimo cha msimu. Zaidi ya hayo, alitangaza ujenzi wa machinjio ya kisasa itakayoongeza thamani ya mifugo na kufungua masoko mapya kwa wafugaji.
Ili kuhakikisha kuwa malighafi za kilimo zinaleta tija zaidi, Dk. Nchimbi alibainisha kuwa Ilani ya CCM imeweka mkazo katika ujenzi wa viwanda. "Tutahakikisha tunajenga viwanda vya kusindika mafuta ya alizeti, viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo kwa kutumia mashudu, na vilevile viwanda vya usindikaji wa mazao mengine, nyama, na maziwa," alieleza Dk. Nchimbi. Mpango huu unalenga kuifanya Singida kuwa kitovu cha uzalishaji na usindikaji, hivyo kutengeneza ajira na kuongeza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.
Kuhusu sekta ya madini, Balozi Nchimbi alihakikishia wachimbaji wadogo kuwa serikali ijayo itakuwa bega kwa bega nao. Alisema mkakati ni kuongeza idadi ya masoko rasmi ya madini ili kuwaondolea adha ya walanguzi na kuwapa bei halali. "Tayari tunalo soko zuri la madini pale Shelui, lakini tunaongeza soko jingine hapa Puma na lingine litafuata. Lengo ni kusogeza huduma karibu na wachimbaji," alisisitiza. Aidha, aliahidi kuwa serikali itaongeza nguvu katika shughuli za utafiti wa madini katika eneo la Ikungi ili kubaini rasilimali zilizopo na kuwawezesha wachimbaji kufanya kazi zao kwa tija na usalama zaidi.