Akitumia lugha ya picha, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, ametoa onyo kali kwa wagombea walioshinda kura za maoni ndani ya chama hicho, akiwataka kuwaunganisha wanachama na kuacha mara moja tabia ya kuwabeza walioshindwa. Wasira alisisitiza kuwa chama hicho ni kama mtumbwi unaobeba watu wengi, na hakitavumilia kuona wachache wakijaribu kuutoboa na kuzamisha wote.
Onyo hilo kali alilitoa mjini Kilosa, Mkoa wa Morogoro, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kampeni za kuwanadi wagombea wa chama hicho kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani.
Wasira alikiri waziwazi kuwepo kwa "misuguano" na sintofahamu katika baadhi ya maeneo baada ya mchakato wa kura za maoni, ambapo walioshindwa na wafuasi wao bado wanaamini hawakutendewa haki. Alisema amekutana na changamoto kama hizo katika maeneo mengine na ilibidi afanye maamuzi magumu, ishara kwamba hatasita kuchukua hatua kama hali hiyo itaendelea.
Hata hivyo, alielekeza agizo lake zito kwa waliopewa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama. "Ninyi mliopewa dhamana ya ushindi mna jukumu kubwa zaidi la kuleta umoja kuliko hata walioshindwa," Wasira alisisitiza. "Ukipata ushindi halafu nawe unaanza kutamba na kujivuna, huku kundi lako likiwatambia wengine, unatufarakanisha na unadhoofisha chama."
Aliwataka wagombea hao kuwa wanyenyekevu na kuchukua hatua ya kwanza kwenda kuwatafuta wale walioshindwa. Aliwakumbusha kuwa uongozi ndani ya CCM ni wa kupokezana na ni kama zamu. "Nendeni mkawaambie wenzetu kwamba leo ni zamu yetu, lakini kesho inaweza kuwa yao. Sote ni wanafamilia moja ya CCM na lengo letu ni kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu," aliongeza.
Ujumbe wake unalenga kuzima makundi na mifarakano ambayo mara nyingi hujitokeza baada ya kura za maoni na ambayo yanaweza kugharimu chama kwenye uchaguzi mkuu kama hayatapatiwa ufumbuzi wa haraka.