Kauli nzito na yenye onyo kali imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, akiwaonya wale wote wenye mpango wa kuingia mitaani kuandamana ifikapo Oktoba 29. Akizungumza kwa kujiamini mbele ya umati mkubwa katika mkutano wa kampeni mjini Karagwe, Bashungwa alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viko imara na havitasita kuchukua hatua. "Nikiwa Waziri unayeniamini," alimweleza mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, "Vyombo vyetu viko timamu kuhakikisha amani inatawala. Hakuna atakayethubutu kuandamana Oktoba 29, atakutana na visiki," alionya Bashungwa huku akiwasihi vijana kutokubali kutumika katika mipango hiyo.
Onyo hilo la Bashungwa lilikuja wakati Dkt. Samia akiendelea na kampeni zake mkoani Kagera, ambapo alitumia fursa hiyo kumwaga ahadi lukuki zinazolenga kuufungua kiuchumi mkoa huo. Akiwa katika wilaya za Muleba, Missenyi, na Karagwe, mgombea huyo wa CCM alieleza dira yake ya kuifanya Kagera kuwa kitovu cha fursa na uwekezaji.
Akiwa Missenyi, aliahidi mradi mkubwa wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa katika eneo la Kyabajwa, utakaokuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa aina ya Boeing, na hivyo kurahisisha usafiri na utalii. Aidha, aliahidi kuliweka zao la vanilla katika ramani ya dunia na kukamilisha ujenzi wa miradi tisa ya maji pamoja na Daraja la Kitengule, kiungo muhimu cha wilaya za Missenyi, Karagwe, na Ngara, mradi utakaogharimu Shilingi bilioni 31.5.
Kwa upande wa Muleba, Dkt. Samia alilenga sekta ya uvuvi na kilimo, akiahidi kutoa boti za kisasa za uvuvi, boti za kubebea wagonjwa katika visiwa vya Goziba na Bumbire, na boti za doria ili kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria. Katika kilimo, alisisitiza kuongeza uzalishaji wa miche ya kahawa kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ambayo tayari inanufaisha vijana 300 katika shamba la ekari 300 mkoani humo.
Wakati kampeni za CCM zikipamba moto Kagera, mgombea mwenza wa urais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akiwa mkoani Singida, aliahidi mapinduzi ya viwanda vya alizeti ili kumaliza tatizo la kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Wakati huo huo, chama cha upinzani cha Sauti ya Umma (SAU), kupitia mgombea wake Majaliwa Kyara, kikiwa Arusha, kiliendelea kuahidi huduma za kijamii kama bima ya afya kwa wote na upatikanaji wa maji safi kila kata.