Akiendeleza kampeni zake za Uchaguzi Mkuu wa 2025, mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa kauli nzito Kisiwani Pemba, akijipambanua kama kiongozi anayechukia na kupinga vikali siasa za ubaguzi wa Upemba na Uunguja. Akizungumza na viongozi wa dini, Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa utawala wake umekuwa na unaendelea kuzingatia uwezo na utendaji kazi kama kigezo pekee cha uteuzi, na si asili ya mtu.
"Mimi ni muumini wa vitendo. Ninapofanya uteuzi wa viongozi, siangalii huyu anatoka Pemba au Unguja. Kigezo changu ni uwezo wa mtu kufanya kazi na kuwatumikia wananchi. Namshukuru Mungu nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuvunja hili," alisema Dk. Mwinyi, akituma ujumbe wa moja kwa moja kwa eneo ambalo kihistoria limekuwa likilalamikia kutengwa.
Alikumbusha jamii juu ya historia ya machungu ya kisiasa Visiwani, ambapo chuki ilipandikizwa hadi kufikia hatua ya watu kugawanyika katika misiba na shughuli za kijamii kwa misingi ya vyama vyao. Alisema hali hiyo sasa ni historia, na amani na maridhiano yaliyopo ni matokeo ya kazi kubwa, ambayo yeye mwenyewe alishiriki kuijenga.
Dk. Mwinyi alirejea jukumu lake muhimu katika kufufua Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya mazungumzo yake na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad. Alisema maridhiano hayo ndiyo yamezaa utulivu unaoshuhudiwa sasa, ambao ni msingi usiokuwa na mbadala wa maendeleo yoyote.
"Hakuna maendeleo bila amani. Umoja wetu unajengwa kwa kutobaguana. Kwa hiyo, nazitaka hoja zozote za kichochezi zinazoibua ubaguzi zipuuzwe kabisa na wananchi wote," alihimiza. Aliahidi kuwa serikali yake itaendelea kuwa ya wote, ikisimamia haki, umoja, na mshikamano kama nguzo kuu za uongozi.