Wakati joto la kisiasa likianza kupanda kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Makini Taifa, Ameir Hassan Ameir, ametupa bomu la aina yake kwenye ulingo wa siasa za Zanzibar. Ametangaza ahadi nzito kwamba endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atahakikisha kila raia Mzanzibari anapokea mshahara wa Shilingi 500,000 kila mwezi.
Ameir alitoa ahadi hiyo ya kipekee leo, Julai 10, 2025, wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) visiwani humo. Cha kushangaza, kikao hicho kilikuwa kinajadili utekelezaji wa Ilani ya Chama tawala cha CCM, lakini Bw. Ameir alitumia fursa hiyo kuweka wazi ajenda ya chama chake endapo kitashika dola.
Akifafanua kuhusu sera hiyo, ambayo kwa mataifa mengine duniani inajulikana kama "Universal Basic Income" (Mshahara wa Msingi kwa Wote), Ameir alisema lengo lake ni kutokomeza umasikini, kupunguza utegemezi, na kuwapa nguvu za kiuchumi vijana na wanawake ili waweze kujiajiri na kujitegemea.
"Wakati umefika wa kujenga Zanzibar yenye heshima, isiyo na ombaomba, na yenye usawa wa kiuchumi. Tunataka kuwapa wananchi wetu mustakabali bora, bila kujali hali zao za sasa," alisema Ameir kwa msisitizo.
Ahadi hii ya Chama Cha Makini Taifa inatajwa kuwa huenda ikabadilisha kabisa mwelekeo wa mijadala ya kisiasa visiwani Zanzibar. Wakati wengine wakiiona kama ahadi isiyotekelezeka au ya "kufuru", wengine wanaweza kuiona kama siasa ya kisasa inayolenga kumweka mwananchi katikati ya maendeleo. Bila shaka, ahadi hii sasa itazilazimu kambi nyingine za kisiasa kujipima na kujibu hoja hii nzito iliyoletwa mezani na Katibu Mkuu huyo.