Dunia imetakiwa kukaa chonjo na kujiandaa kwa mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya mwanadamu. Kampuni ya OpenAI, wababe walio nyuma ya teknolojia maarufu ya ChatGPT, wametoa wito mzito kwa serikali, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla kuunganisha nguvu kujiandaa na ujio wa 'Superintelligence'—aina mpya ya Akili Mnemba (AI) yenye uwezo unaopitiliza akili ya kawaida ya binadamu.
Katika andiko lao la hivi karibuni, OpenAI wameeleza kuwa ingawa kwa sasa tunaweza kuona maisha yakiendelea kama kawaida kutokana na mazoea yetu ya kila siku, ukweli ni kwamba teknolojia imepiga hatua kubwa mno ndani ya muda mfupi. Wengi bado wanaichukulia AI kama kijifaa cha kurahisisha kazi ndogondogo tu, lakini uwezo wake halisi ni mkubwa zaidi. Wamebainisha kuwa gharama za kuendesha mifumo hii zinashuka kwa kasi ya ajabu—kama vile bei ya bidhaa muhimu ingekuwa inashuka mara 40 kila mwaka!
Utabiri wao unasisimua na kutisha kwa wakati mmoja. OpenAI wanaamini kuwa kuanzia mwaka kesho, AI itaanza kufanya uvumbuzi wake yenyewe, japo kwa kiwango kidogo. Lakini ifikapo mwaka 2028 na kuendelea, tutatarajia kuona mifumo ya AI ikifanya uvumbuzi mkubwa wa kisayansi ambao unaweza kubadilisha kila sekta. Hapa ndipo tunapoelekea kwenye 'Artificial General Intelligence' (AGI), hatua ambayo mashine zitakuwa na uwezo wa kujifunza na kujiboresha zenyewe.
Kutokana na kasi hii, OpenAI inapendekeza ushirikiano wa dhati ili kuepusha majanga. Wanataka kuwepo na kanuni za pamoja za usalama kati ya kampuni kubwa za teknolojia, sawa na jinsi tunavyo na sheria za ujenzi ili kuzuia nyumba kuporomoka, au itifaki za usalama wa mtandao zinazolinda mifumo yetu ya kifedha. Wanaonya kuwa sheria za kawaida za serikali hazitatosha kudhibiti teknolojia yenye uwezo wa kujiongeza yenyewe au inayoweza kutumika vibaya katika matukio kama ya ugaidi wa kibiolojia.
Ujumbe wao mkuu ni kwamba, ndani ya miaka michache ijayo, AI haitakuwa tena kitu cha anasa kwa wachache. Itageuka kuwa huduma ya msingi kabisa inayohitajika kwa maisha ya kila siku, sawa na umuhimu wa maji safi au umeme wa uhakika. Hivyo, ujenzi wa miundombinu ya kuimudu teknolojia hii si jukumu la makampuni pekee, bali ni suala la kitaifa na kidunia. Mkurugenzi wa OpenAI, Sam Altman, amesisitiza uzito wa jambo hili, akiashiria kuwa tuko ukingoni mwa mapinduzi mapya ya kifikra na kiuchumi.