Ndoto ya karne nyingi ya wataalamu wa zamani wa alkemia (alchemy) ya kubadilisha madini ya kawaida kama risasi kuwa dhahabu hatimaye imefikiwa na wanafizikia wa kisasa. Timu ya watafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Nyuklia ya Ulaya (CERN) imefanikiwa kwa mara ya kwanza kwa utaratibu wa kisayansi kugeuza risasi kuwa dhahabu kwa kutumia mashine yao kubwa iitwayo Large Hadron Collider (LHC). Matokeo ya utafiti huu wa kusisimua yalichapishwa hivi karibuni, tarehe 7 Mei 2025, katika jarida maarufu la kisayansi liitwalo 'Physical Review Journals'.
Tangu karne ya 17, wanasayansi na wataalamu wa alkemia walijaribu bila mafanikio kubadilisha risasi, ambayo hupatikana kwa wingi duniani, kuwa dhahabu, madini adimu na ya thamani. Tatizo kubwa lililowakabili ni tofauti ya msingi katika muundo wa atomi za madini hayo mawili. Kila atomi ina kiini chenye chembechembe ndogo ziitwazo protoni na nyutroni. Idadi ya protoni ndiyo huamua aina ya elementi. Risasi ina protoni 82 katika kiini chake, wakati dhahabu ina protoni 79. Hivyo, ili kugeuza risasi kuwa dhahabu, inahitajika kuondoa protoni tatu kutoka kwenye kiini cha atomi ya risasi.
Watafiti wa CERN, wakitumia LHC – ambayo ni maabara kubwa zaidi duniani ya majaribio ya kisayansi – waliweza kufanikisha hili. LHC, iliyojengwa nchini Ufaransa mpakani na Uswizi, ni mzunguko mkubwa wa kilomita 27 uliofukiwa mita 100 chini ya ardhi. Mashine hii hutumika kuongeza kasi ya chembechembe za atomi hadi kufikia karibu na kasi ya mwanga, na kisha kuzigonganisha ili kuchunguza matokeo yake na kugundua chembechembe mpya.
Katika jaribio hili, watafiti walielekeza miale ya fotoni (chembe za mwanga) zenye nishati kubwa sana kuelekea kwenye atomi za risasi, zikisafiri kwa kasi inayokaribia ile ya mwanga. Miale hii ilipogongana na atomi za risasi, au hata kupita karibu nazo, ilizalisha uga wenye nguvu nyingi wa sumakuumeme. Uga huu ulisisimua kiini cha atomi za risasi na kusababisha viini hivyo kutoa protoni tatu. Mara tu protoni tatu zilipoondoka, atomi ya risasi (yenye protoni 82) ilibadilika papo hapo na kuwa atomi ya dhahabu (yenye protoni 79).
Kati ya mwaka 2015 na 2018, watafiti wanakadiria kuwa takriban viini vya atomi za dhahabu bilioni 86 viliundwa kupitia migongano iliyotokea kwenye LHC. Hata hivyo, kiasi hiki cha dhahabu ni kidogo mno, kikiwa ni sawa na sehemu moja ya trrilioni 29 ya gramu moja (takriban 1/29×10
−12
g). Zaidi ya hayo, atomi hizi za dhahabu zilizoundwa zilikuwa si thabiti na ziliweza kudumu kwa muda mfupi sana, takriban mikrosekunde moja (sehemu moja ya milioni ya sekunde), kabla ya kugonga kuta za chombo cha majaribio au kubadilika kuwa chembe nyingine.
Uliana Dmitrieva, mmoja wa watafiti wa CERN, alielezea umuhimu wa matokeo haya akisema, "Hii ni mara ya kwanza kwa mchakato wa kubadilisha risasi kuwa dhahabu katika LHC kufanywa kwa njia ya majaribio na kwa utaratibu maalumu na kuchunguzwa kisayansi."
Lengo kuu la utafiti huu si kuzalisha dhahabu kwa wingi ili kupata utajiri, kwani kiasi kinachozalishwa ni kidogo mno na gharama ya mchakato ni kubwa mno kuliko thamani ya dhahabu yenyewe. Badala yake, timu ya watafiti inasema kuwa, "Kuelewa vizuri jinsi miale hii inavyoweza kubadilisha viini vya atomi kutasaidia kuboresha utendaji kazi wa mashine ya LHC." Hivyo, mafanikio haya ni hatua muhimu katika kuelewa zaidi fizikia ya nyuklia na nguvu za msingi zinazounda ulimwengu wetu, na kutimiza ndoto ya karne nyingi kwa njia ya sayansi ya kisasa.