Kampuni ya teknolojia ya Apple, maarufu kwa simu zao za iPhone, inaonekana imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa ambayo huenda yakabadilisha kabisa jinsi tunavyotumia simu zetu za mkononi. Ikiwa umezoea kutafuta mtandao kwa kuinua simu juu ukiwa kijijini au safarini porini, Apple wako mbioni kufanya hilo liwe historia. Taarifa za hivi punde zinaonyesha kuwa kampuni hiyo inapanga kupanua matumizi ya teknolojia ya setilaiti (vyombo vya anga) kwenye simu zake, siyo tu kwa dharura, bali kwa matumizi ya kila siku kama kutuma picha, meseji na hata kutumia ramani.
Mkakati huu mpya unalenga kupunguza utegemezi kwa makampuni ya simu (kama tunavyoyajua hapa nchini). Badala ya kusubiri minara ijengwe kila kona, Apple wanataka simu yako iweze kuwasiliana moja kwa moja na setilaiti angani. Hii ina maana siku za usoni, unaweza kuwa katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti au Ruaha, ukiwa hauna 'network' kabisa ya kawaida, lakini bado ukaweza kutuma picha zako za 'selfie' kwa wapendwa wako mjini.
Mwandishi maarufu wa masuala ya teknolojia, Mark Gurman wa Bloomberg, amefichua kuwa huu ni mpango ambao Apple wamekuwa wakiufanyia kazi kwa kimya kimya kwa takriban miaka 10 sasa. Walianza kidogo na iPhone 14 mwaka 2022 kwa kuweka huduma ya SOS ya dharura kupitia setilaiti, lakini hiyo ilikuwa ni 'kionjo' tu.
Sasa, wamepania kufanya makubwa zaidi. Mipango iliyopo mezani ni pamoja na kuruhusu programu nyingine (kama WhatsApp au Instagram huko mbeleni) kutumia mfumo huu wa setilaiti, na kuboresha programu yao ya ramani (Apple Maps) ili ifanye kazi hata bila mtandao wa data. Kibwagizo kikubwa zaidi ni teknolojia mpya inayofanyiwa kazi ambayo itakuondolea adha ya kulazimika kunyoosha mkono angani kutafuta setilaiti; simu itaweza kuunganishwa hata ikiwa mfukoni au ndani ya gari.
Ili kufanikisha hili, Apple wamewekeza kiasi kikubwa cha fedha, kinachokadiriwa kufikia mabilioni ya Shilingi za Kitanzania, kwa mshirika wao mkuu wa miundombinu ya anga, kampuni ya Globalstar. Hata hivyo, biashara hii ina ushindani mkali. Bilionea Elon Musk kupitia kampuni yake ya SpaceX naye ananyemelea kununua Globalstar, huku akiwa tayari ameshaanza ushirikiano na kampuni ya T-Mobile kutoa huduma zinazofanana.
Huu ni mchezo wa muda mrefu wa Apple, kuhakikisha wanashikilia kila kitu kuanzia kifaa mkononi mwako hadi mtandao unaokupa mawasiliano, wakilenga kukupa uhuru wa kuwasiliana popote duniani bila mipaka.