Wanasayansi kutoka Urusi wamefanya ugunduzi wa kushangaza katika Bahari ya Kaspi, eneo kubwa zaidi la maji baridi duniani, baada ya kubaini kuibuka kwa kisiwa kipya kaskazini mwa bahari hiyo. Ugunduzi huu umethibitishwa na Shirika la Habari la Urusi, TASS, likionyesha jinsi mabadiliko ya kiwango cha maji yanavyoweza kusababisha matukio ya kijiografia. Kisiwa hiki kipya kipo takriban kilomita 30 kusini-magharibi mwa Kisiwa cha Maly Zhemchuzhny. Wakati wa ugunduzi wake, eneo la kisiwa hicho lilikuwa na unyevu, lenye usawa mkubwa, na lilifunikwa na matuta ya mchanga, ikionyesha asili yake ya kitope.
Kwa sasa, kisiwa hicho kimeinuka kidogo tu juu ya usawa wa maji, na uwepo wake unahusishwa moja kwa moja na kupungua kwa kina cha maji katika Bahari ya Kaspi. Dk. Stepan Podoliako, mtafiti mkuu kutoka Taasisi ya Oceanology ya Chuo cha Sayansi cha Urusi (IO RAS), amethibitisha kuwa kuibuka kwa visiwa vipya katika Bahari ya Kaspi kunahusiana na mabadiliko ya muda mrefu ya kiwango cha maji katika bahari hiyo ya ndani. Alieleza kuwa visiwa vya aina hii huibuka wakati kiwango cha maji kinapungua, na hivyo kufichua miinuko ya chini ya bahari.
Bahari ya Kaspi, iliyo kwenye makutano ya Ulaya na Asia, ina eneo la takriban kilomita za mraba 371,000, na kuifanya kuwa eneo kubwa zaidi la maji la ndani duniani. Dk. Podoliako alifafanua kuwa viwango vya maji katika Bahari ya Kaspi vimekuwa vikishuka na kupanda mara kadhaa katika historia, ikiwemo kushuka katika miaka ya 1930 na 1970 kabla ya kupanda tena. Hata hivyo, tangu takriban mwaka 2010, kiwango cha maji kimeanza kushuka tena. Aliongeza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuwa sababu kuu ya kupungua huku kwa hivi karibuni, hasa kwa sababu kiwango cha maji kinategemea kwa kiasi kikubwa uvukizaji.
Wanasayansi waligundua kwa mara ya kwanza ishara za kisiwa hiki kupitia picha za satelaiti mwezi Novemba 2024. Ingawa matuta ya mchanga na mabaki ya ardhi yalikuwa yameanza kuonekana na kukauka juu ya usawa wa maji, baadhi ya wataalamu walikuwa na mashaka iwapo ingeweza kuitwa rasmi kisiwa kipya. Hivi karibuni, watafiti walijaribu kufika kisiwani hapo kuthibitisha uwepo wake, lakini walishindwa kutokana na hali mbaya ya hewa na kina kifupi cha maji. Hata hivyo, waliweza kutumia droni kuthibitisha ukubwa na baadhi ya sifa za kisiwa hicho. Utafiti zaidi unahitajika ili kuelezea kwa undani sifa zake, na Dk. Podoliako amefichua kuwa ziara nyingine kisiwani hapo imepangwa kufanyika nusu ya pili ya mwaka 2025. Hili linaashiria hatua muhimu katika kuelewa mienendo ya kipekee ya Bahari ya Kaspi na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.