Dunia ya teknolojia inazidi kwenda kasi kuliko daladala za Mbagala Rangi Tatu asubuhi. Kampuni ya Google, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ndiyo 'kamusi' na 'maktaba' yetu kuu, imeamua kufanya mabadiliko ambayo yatafuta kabisa mazoea yetu ya kutafuta vitu mtandaoni (Searching). Katika tangazo jipya lililotolewa tarehe 2 Desemba, Google imeweka wazi kuwa inaanza jaribio la kimataifa la kuunganisha mfumo wake wa kutafuta na Akili Mnemba (AI) ili kufanya uzoefu wa mtumiaji uwe wa kipekee.
Kwa lugha nyepesi, kile kitendo cha kuandika neno moja au mawili (Keywords) na kupewa orodha ya viungo (links) kinaelekea ukingoni. Sasa, Google inataka uongee nayo kama unavyoongea na rafiki yako.
Muunganiko wa 'AI Overview' na 'AI Mode'
Mkakati huu mpya unahusisha kuunganisha vitu viwili vikubwa: 'AI Overview' (Muhtasari unaotolewa na AI juu ya majibu) na 'AI Mode' (Mfumo wa maongezi).
Hapo awali, ukigoogle kitu, ungepata majibu, na kama ungetaka kuuliza swali la nyongeza, ilibidi ubonyeze kitufe kingine kuingia kwenye 'AI Mode'. Sasa, ukuta huo umepomolewa. Ukishapata jibu la kwanza, utaweza kuendeleza maongezi hapohapo bila kuhama.
Robby Stein, Makamu wa Rais wa Google, amefafanua falsafa hii mpya kupitia mtandao wa X: "Mtumiaji hapaswi kuumiza kichwa wapi au vipi aulize swali. Lengo letu ni kukupa taarifa muhimu kupitia AI Overview, na kisha kukuruhusu uulize maswali ya nyongeza hapohapo... liwe swali refu, fupi, au gumu, wewe uliza tu."
Kwanini Google Inabadilika?
Wataalamu wa Google wamegundua tabia moja ya kibinadamu: Mara nyingi tunapoingia Google, hatuna uhakika tunataka nini hasa. Mtu anaweza kuandika "Simu ya Tecno" akimaanisha anataka kujua bei, lakini kumbe moyoni anataka kujua kama kamera yake ni nzuri au inadumu na chaji.
Mfumo huu mpya umeundwa "kudaka" mawazo hayo. Hata kama utaanza na swali la kijinga au lisiloeleweka, Google itakujibu na kukupa mwanya wa kufafanua zaidi, kama vile unavyopiga stori na mshikaji wako ambaye anakuelewa hata ukiongea kwa mkato.
Vita ya Wababe: Google vs OpenAI
Hatua hii haijaja kwa bahati mbaya. Ni jibu la kibabe dhidi ya washindani wao, OpenAI (wamiliki wa ChatGPT). Wakati OpenAI wakiwa wamewasha "Taa Nyekundu" (Code Red) wakihofia kupitwa na teknolojia mpya ya Google ya 'Gemini 3', Google inazidi kutanua wigo.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwezi Novemba pekee, Google imefikisha watumiaji hai (Active Users) milioni 650 kwenye mifumo yake ya Gemini na 'Nano Banana'. Ikumbukwe kuwa kipengele cha 'AI Overview' pekee kinatumiwa na watu bilioni 2 kila mwezi duniani. Hivyo, kwa kuunganisha huduma hizi, Google inataka kuhakikisha watumiaji hawaendi kokote.
Mwisho wa 'Search', Mwanzo wa 'Chat'
Hii ni hatua kubwa ya kimapinduzi. Tunahama kutoka kwenye "Utafutaji wa Maneno" (Keyword-based search) kwenda kwenye "Utafutaji wa Maongezi" (Conversation-based search). Mipaka kati ya 'Search Engine' na 'Chatbot' inafutika rasmi.
Kwa watumiaji wa simu janja nchini Tanzania, hii inamaanisha urahisi zaidi. Badala ya kufungua kurasa kumi kusoma habari moja, utamalizana na Google hapohapo kwenye ukurasa wa mwanzo. Google inasema itapanua wigo wa huduma hii kulingana na matokeo ya majaribio haya, hivyo kaa mkao wa kula, simu yako inakaribia kuwa na akili zaidi.