Kama ulikuwa unategemea "dezo" ya Akili Mnemba (AI) ili kutengeneza video kali za Instagram au picha za matangazo ya biashara yako, anza kujipanga upya. Zama za "vya bure" zinaelekea ukingoni kwa kasi ya ajabu. Vigogo wa teknolojia duniani, Google na OpenAI, wametangaza hatua mpya za kukaza vyuma kwa watumiaji wa bure wa mifumo yao maarufu ya 'Nano Banana Pro' na 'Sora', wakidai kuwa mitambo yao inalemewa na mzigo wa watumiaji ("Server Overload").
Hii ni habari mbaya kwa vijana wa "Silicon Dar" na waundaji maudhui (Content Creators) hapa Tanzania ambao wamekuwa wakitumia zana hizi kama mbadala wa gharama kubwa za utengenezaji video na picha (Production).
"GPU Zinayeyuka Kama Barafu"
Bill Peebles, Mkuu wa Kitengo cha Sora pale OpenAI (kampuni inayomiliki ChatGPT), ametoa kauli iliyozua mjadala mzito mtandaoni. Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) tarehe 28, Peebles aliandika kwa lugha ya picha: "GPU zinayeyuka (GPUs are melting)."
Hii haina maana kwamba kompyuta zinaungua moto halisi, bali ni lugha ya kitaalamu inayoashiria kuwa mitambo ya kuchakata data (Servers) imezidiwa kiasi cha kupitiliza kutokana na maombi mamilioni ya kutengeneza video yanayoingia kila sekunde.
Kutokana na hali hiyo, OpenAI imetangaza rasmi kuwa watumiaji wa bure wa mfumo wa Sora (unaotengeneza video kwa maandishi) sasa wataruhusiwa kutengeneza video sita (6) tu kwa siku. Hii ni dozi ndogo sana ukilinganisha na uhuru uliokuwepo awali.
Peebles ameongeza kuwa huu si mpango wa muda mfupi, bali ndio utaratibu mpya wa kudumu. "Kama unahitaji zaidi, itabidi ununue," alisisitiza. Hii inaashiria kuanzishwa kwa mfumo mpya wa malipo unaotegemea matumizi (Pay-per-use), tofauti na ule wa usajili wa mwezi (Subscription).
Google Nayo Yakaza Kamba
Wakati OpenAI wakilia na video, Google nao wanalia na picha. Mfumo wao mpya na maarufu wa kutengeneza picha, 'Nano Banana Pro', nao umekumbwa na panga.
Google imetangaza kupunguza idadi ya picha za bure ambazo mtumiaji anaweza kutengeneza kwa siku kutoka picha tatu (3) hadi picha mbili (2) tu. Ingawa inaonekana kama punguzo dogo, Google wametoa angalizo kuwa: "Kutokana na mahitaji makubwa, kikomo hiki cha kila siku kinaweza kubadilika muda wowote." Hii ina maana kuwa kesho unaweza kuamka na kukuta unaruhusiwa picha moja au hakuna kabisa.
Wanafunzi na Watafiti Hatarini
Pigo lingine limeenda kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na watafiti wanaotumia 'NotebookLM'. Huu ni mfumo wa Google unaosaidia kusoma na kuchambua nyaraka. Google imezuia watumiaji wa bure kutumia vipengele vipya vya 'Infographics' (Chati za Taarifa) na 'Slide Decks' (Slaidi za kuwasilisha mada) ambazo zinaendeshwa na Nano Banana Pro. Hata wale wanaolipia kifurushi cha 'Pro' wamewekewa vikwazo vya ziada.
Hali hii pia imeathiri mfumo wa 'Gemini 3 Pro', ambapo ile ofa ya awali ya kuingiza maagizo (prompts) matano na picha tatu kwa siku imefutwa, na badala yake imebaki kile wanachoita "Ufikiaji wa Msingi" (Basic Access), lugha ambayo kimsingi inamaanisha huduma imepunguzwa makali.
Kwanini Hii Inatokea Sasa?
Wataalamu wa uchumi wa kidijitali wanasema hii ilitarajiwa. Gharama ya kuendesha mitambo ya AI ni kubwa mno. Umeme unaotumika kupoza seva (Servers) na gharama za vipuri (Chips za NVIDIA) ni mzigo mkubwa kwa makampuni haya.
Mkakati wao ulikuwa ni kutoa huduma bure mwanzoni ili "kunasa" watumiaji (Customer Acquisition), na sasa baada ya watu kuzoea na kuwa 'teja' wa huduma hizo, wameanza kutoza. Ni kama vile muuza 'supu' anavyokupa onja-onja mwanzoni, ukishapenda ladha, unalipia bakuli zima.
Ushauri kwa Watanzania
Hali hii inatukumbusha kuwa katika ulimwengu wa biashara, hakuna cha bure cha kudumu. Kwa wabunifu wa picha (Graphics Designers) na Wahariri wa Video hapa nchini, huu ni wakati wa kuanza kuweka bajeti ya kulipia zana hizi kama sehemu ya gharama za uendeshaji (Operational Costs).
Kutegemea akaunti za bure kunaweza kukukwamisha katikati ya kazi ya mteja. Pia, ni fursa ya kuanza kutafuta njia mbadala au kujifunza kutumia mifumo ambayo ni 'Open Source' (Chanzo Huria) ambayo inaweza kupunguzia makali ya gharama.
Kama wahenga walivyosema, "Mgeni njoo, mwenyeji apone," lakini kwa Google na OpenAI, mgeni (mtumiaji wa bure) sasa anaambiwa "Toa pesa auupishe kiti."