Akili Unde Isiwatishe: Chuo cha Ustawi wa Jamii Chawapa Mbinu Wasomi "Kuchakarika" na Teknolojia Mpya

it | Fri Dec 19 2025


Akili Unde Isiwatishe: Chuo cha Ustawi wa Jamii Chawapa Mbinu Wasomi "Kuchakarika" na Teknolojia Mpya

Katika ulimwengu wa sasa ambapo kasi ya teknolojia inabadilika kama upepo, Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW) jijini Dar es Salaam kimeamua kuwawahi wahitimu na wanafunzi wake kwa kuwapa "silaha" mpya za kidijitali. Katika Kongamano la 12 la taaluma hiyo lililofanyika leo, msisitizo mkubwa umewekwa kwenye matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) kama nyenzo ya kurahisisha utendaji kazi badala ya kuiona kama tishio la kupokonya ajira.


Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk. Joyce Nyoni, akifungua kongamano hilo lenye msisimko wa kipekee, amewataka wasomi nchini kuachana na hofu ya kizamani kuwa mashine zitachukua nafasi za binadamu. Badala yake, amewahimiza kuichukulia AI kama "msaidizi wa kazi" (personal assistant) ambaye ana uwezo wa kuchakata taarifa nyingi kwa muda mfupi.


"Tulipoanza kusikia habari za Akili Mnemba kama nchi, kulikuwa na hofu kubwa kwamba fursa za ajira zingetoweka na wahitimu wetu kubaki vijiweni. Lakini leo, tunawafumbua macho kuwa AI haiwezi kuchukua nafasi ya mwanadamu mwenye weledi; badala yake, ni fursa kwa mtaalamu kuitumia ili kuongeza ufanisi na ubunifu katika kutoa huduma kwa jamii," alisema Dk. Nyoni huku akishangiliwa na mamia ya wanafunzi.


Hata hivyo, Dk. Nyoni ametoa angalizo la msingi kwa wahitimu hao: AI isitumike kama kichaka cha uvivu. Amewataka wanafunzi kutumia teknolojia hiyo kwa kufuata misingi ya weledi na maadili ya kazi, wakitambua kuwa uwezo wa mwanadamu kufikiri kwa kina (critical thinking) bado ni injini kuu ya maendeleo. "Msiwe watu wa kuhamisha tu (copy and paste) kile mnachokipata kwenye mifumo hiyo, bali kitumieni kuchakata taarifa ili kuleta majibu yenye tija," alisisitiza.


Kwa upande wake, Dk. Hellen Maziku, ambaye alikuwa mtoa mada mkuu katika kongamano hilo, aligusia kiini cha taaluma ya ustawi wa jamii akibainisha kuwa AI haina "moyo." Alifafanua kuwa ingawa AI inatumika duniani kote kwa kasi ya ajabu, bado haiwezi kuchukua nafasi ya maofisa ustawi wa jamii kwa sababu kazi hizo zinahusisha hisia, huruma, na uelewa wa hali ya juu wa utu wa mwanadamu – vitu ambavyo teknolojia haina.


"Tunapaswa kubadilisha mtazamo wetu (mindset). AI haifikiri kama binadamu na haitambui hisia za mtu anayepitia changamoto za kisaikolojia. Hivyo, wakati tunatumia teknolojia hii kurahisisha ripoti na takwimu, lazima tubaki na ule upande wetu wa ubinadamu. Ni lazima tubadilike kwa sababu teknolojia hii haiepukiki," aliongeza Dk. Maziku.


Kongamano hili limeacha ujumbe mzito kwa vijana wa Kitanzania: Teknolojia si adui, bali ni daraja la kufikia ufanisi wa kimataifa iwapo itatumiwa kwa akili na uzalendo.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.