Kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwake mnamo Julai Mosi, 2025, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umefanya mafunzo muhimu Jijini Dar es Salaam, yakilenga kuongeza uelewa na kuboresha utendaji kazi katika sekta binafsi na umma. Mafunzo haya yamewajengea uwezo wadau kuhusu masuala muhimu ya usalama na afya mahala pa kazi, sambamba na kuwafunza jinsi ya kuwasilisha madai ya fidia kwa ufanisi zaidi kupitia mifumo ya kidijitali.
Akifungua rasmi mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk. Abdulsalaam Omar, ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini, alisisitiza umuhimu wa mafunzo haya katika kuwajengea uwezo waajiri na wawakilishi wao. Alieleza kuwa mkutano huu unatoa fursa ya kipekee ya kubadilishana mawazo na kukumbushana umuhimu wa kutambua na kudhibiti vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kutokea maeneo ya kazi. "Tunakutana na maafisa rasilimali watu, maafisa usalama na afya ili kuwakumbusha namna ya kubaini vihatarishi, na pale ajali au magonjwa yanapotokea, jinsi ya kuwasilisha madai mapema," alifafanua Dk. Omar. Aidha, aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga pia kuongeza uelewa wa jinsi ya kufanya uchunguzi wa kina wa ajali zinazotokana na kazi na namna bora ya kuzidhibiti ili zisijirudie.
Washiriki wa mafunzo hayo walionyesha kuridhishwa na yaliyomo. Bwana Hamid Shebuge, Meneja kutoka kiwanda cha sukari Bagamoyo, alipongeza WCF kwa kuleta programu ya "Vision Zero." Alifafanua kuwa mpango huu unalenga kuwaelimisha wafanyakazi na menejimenti juu ya wajibu wao katika kulinda usalama wa watu na miundombinu. "Kupitia programu hii, sisi kiwandani kwetu tumepata elimu tunayoendelea kuifanyia kazi. Tunashukuru WCF kwa miaka kumi ya huduma endelevu," alisema Shebuge.
Naye George Alando kutoka DSM Corridor Group alisisitiza jinsi mafunzo hayo yalivyoweka msisitizo mkubwa kwenye matumizi ya teknolojia (TEHAMA) katika kuwasilisha madai ya fidia kwa wafanyakazi wanaopatwa na ajali. Aliongeza kuwa walijifunza kwa kina sheria zinazoongoza WCF, ikiwemo masuala ya usalama kazini, na jinsi waajiri na waajiriwa wanavyopaswa kuzingatia na kuelimishana juu ya masuala hayo muhimu.
Bi. Jill Kaijage kutoka TIPER, alieleza kuwa mafunzo hayo yaliwasaidia sana waajiri kuelewa sheria zinazosimamiwa na WCF. "Tumeweza kubaini changamoto zinazoweza kutokea endapo mwajiri atakuwa hajalipa michango kwa wakati, na pindi mfanyakazi anapopatwa na madhila. Tumefahamu pia taratibu zinazofuatwa na WCF, pamoja na sheria zinazohusu waajiri wasiotoa taarifa sahihi za wafanyakazi wao," alifafanua Bi. Kaijage.
Kwa upande wake, Julieth Joseph kutoka Ensol Tanzania Limited, alieleza jinsi alivyojifunza mambo mengi, ikiwemo umuhimu wa kuzuia ajali na magonjwa badala ya kusubiri yatokee. "Nimevutiwa zaidi na jinsi WCF wanavyotumia mifumo ya mtandaoni kurahisisha uwasilishaji wa taarifa, jambo linalosaidia sana katika utunzaji wa kumbukumbu," alisema Bi. Joseph.
Kwa ujumla, mafunzo haya yaliyofanywa na WCF yana lengo la kuendelea kutoa uelewa mpana kuhusu huduma zao, umuhimu wa usalama na afya mahala pa kazi, sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, na hatua sahihi za kufuata wakati wa kuwasilisha madai ya fidia, hususan kupitia njia ya mtandaoni. Hii inaashiria azma ya WCF ya kuendelea kuboresha huduma zao na kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi nchini Tanzania.