Zaidi ya watu 20 wamejeruhiwa, watatu kati yao vibaya, baada ya ndege tundikizi (swing ride) ya pinduapindua inayoitwa ‘360 Big Pendulum’ kuanguka katika bustani ya burudani nchini Saudi Arabia. Shirika la habari la Marekani, CNN, liliripoti kuwa ajali hiyo ilitokea Julai 30, 2025, katika mji wa Taif, karibu na Jeddah.
Video zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha tukio hilo la kutisha ambapo ndege hiyo ilikuwa ikizunguka hewani kabla ya sehemu ya kubebea watu kugonga sehemu nyingine ya chuma na kuanguka chini kwa kasi kubwa. Kufuatia ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Taif, Saud bin Nahar bin Saud bin Abdulaziz, aliamuru bustani hiyo ya burudani ifungwe mara moja na uchunguzi wa kina uanzishwe ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Ajali hii inatukumbusha umuhimu wa usalama katika vituo vya burudani, na Serikali za nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania, huwa na mamlaka husika zinazokagua na kusimamia usalama wa vifaa hivi ili kuepusha majanga kama haya. Tukio hili linatukumbusha kwamba, wakati mwingine, vitu vinavyokusudiwa kwa ajili ya starehe vinaweza kugeuka kuwa hatari.