Video inayosambaa kwa kasi kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo nchini China imeibua mjadala mkali, ikionyesha jinsi mgahawa maarufu wa kimataifa wa McDonald's uliopo katika barabara ya Siping jijini Shanghai unavyogeuka kuwa makazi ya dharura kwa watu wasio na pa kwenda ifikapo usiku.
Kanda hiyo ya video, iliyosambazwa Septemba 7, inawaonyesha watu kadhaa wakiwa wamelala fofofo kwenye viti vya mgahawa huo. Wengine wamevua viatu na kuunganisha viti viwili au vitatu ili kutengeneza kitanda cha muda, wakijipumzisha bila kujali shughuli zinazoendelea. Mgahawa huu, unaofanya kazi kwa saa 24, umekuwa kimbilio kwa watu ambao aidha wamechelewa kurudi makwao au hawana kabisa mahali pa kulala.
Hali hii imesababisha kuzuka kwa jina jipya miongoni mwa Wachina: "Makimbilio ya McDonald's" au "Wakimbizi wa McDonald's" (McRefugees). Hili ni jambo linaloashiria changamoto kubwa ya kijamii katika majiji makubwa duniani, ambapo gharama za maisha ziko juu na fursa za makazi salama ni chache kwa baadhi ya watu. Migahawa hii inayofunguliwa usiku kucha hutoa usalama, mwanga na wakati mwingine viyoyozi, na kuifanya kuwa chaguo bora kuliko kulala barabarani.
Kwenye mtandao wa Weibo, maoni ya watu yamegawanyika. Wapo walioonyesha kuchukizwa, wakitoa maoni kama, "Viti hivyo lazima vitakuwa vimejaa magonjwa ya ngozi kama vile 'ukurutu'," huku wengine wakitania kwa kejeli, "Suluhisho ni kuwasha joto kali wakati wa kiangazi na baridi kali wakati wa baridi."
Hata hivyo, wapo wengine walioona hali hiyo kama ishara ya tatizo kubwa zaidi la kijamii. Baadhi walitabiri kuwa huenda matukio kama haya yakasababisha usimamizi wa mgahawa huo kuamua kusitisha huduma ya saa 24, jambo ambalo lingewaathiri zaidi watu hao wanaoutumia kama kimbilio lao pekee la usiku.