Hali ya taharuki na mtafaruku imelikumba jiji la Bangkok, mji mkuu wa Thailand, baada ya sehemu kubwa ya barabara kuu ya lami nne kuzama ghafla na kusababisha shimo kubwa (sinkhole), na hivyo kusitisha shughuli za usafiri na kulazimisha maelfu ya watu kuhama makazi na maeneo yao ya kazi.
Tukio hilo la kutisha lilitokea jana, Septemba 24, 2025, majira ya asubuhi katika wilaya ya Dusit, magharibi mwa jiji hilo, mbele ya Hospitali ya Vajira. Shimo hilo lina ukubwa wa kutisha, likikadiriwa kuwa na upana wa mita 30, eneo la mita za mraba 900, na kina cha takriban mita 50 kwenda chini. Ingawa hakuna vifo wala majeruhi vilivyoripotiwa, magari matatu yaliharibiwa baada ya kuanguka ndani ya shimo hilo.
Gavana wa Bangkok, Chadchart Sittipunt, alieleza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa maafa hayo yamesababishwa na kazi za ujenzi wa kituo cha treni ya chini ya ardhi (subway) unaoendelea katika eneo hilo. Mamlaka zimeonya kuwa ardhi inayozunguka eneo la tukio bado haijatulia na inaendelea kusogea, jambo lililosababisha uharibifu kwenye nguzo za jengo la kituo cha polisi kilicho karibu na eneo hilo.
Kutokana na hatari hiyo, mamlaka zimeamuru uhamishaji wa watu katika maeneo ya karibu. Licha ya jengo la Hospitali ya Vajira kutokuwa limeathirika moja kwa moja, wagonjwa wapatao 3,500 waliokuwa wamelazwa hospitalini humo walihamishwa kama tahadhari. Aidha, maafisa wa polisi na wakazi wa majengo jirani nao wameamriwa kuondoka. Jiji la Bangkok limethibitisha kukata huduma za umeme na maji katika eneo hilo ili kuhakikisha usalama.
Kufuatia tukio hilo, uongozi wa Hospitali ya Vajira umetangaza kusitisha huduma zote za wagonjwa wa nje kwa muda wa siku mbili ili kuruhusu tathmini ya usalama na utulivu wa miundombinu inayozunguka hospitali hiyo.