Taasisi ya Al-Hikma Kudhamini Vijana 200 Wasio na Uwezo wa Kulipia Mahari

international | Fri Mar 21 2025


Taasisi ya Al-Hikma Kudhamini Vijana 200 Wasio na Uwezo wa Kulipia Mahari

Taasisi ya Al-Hikma imetangaza kudhamini vijana 200 wasio na uwezo wa kulipia mahari. Lengo ni kuwasaidia kuingia katika ndoa na kuachana na ukapera na tabia zisizofaa.


Tangazo hilo limetolewa jana, Machi 20, 2025, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Shekhe Nurdin Kishki, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.


Shekhe Kishki alisema kuwa taasisi hiyo imeamua kujitoa kwa jamii kwa kusaidia vijana wenye uhitaji wa ndoa lakini wanakabiliwa na changamoto za kifedha.


"Kijana yeyote anayehitaji kuoa lakini hana uwezo wa kulipia mahari au ana uwezo mdogo, anakaribishwa kufika katika ofisi zetu kuchukua fomu isiyokuwa na gharama yoyote, kuijaza na kuirejesha kwa ajili ya usaili. Wale watakaobahatika kupita kwenye udahili, watagharamiwa shughuli yao ya ndoa," alisema Shekhe Kishki.


Alibainisha kuwa udhamini huu unafanyika kwa mwaka wa tatu mfululizo, ambapo idadi ya wanufaika imeongezwa. Kwa mwaka huu, mpango huo utawajumuisha pia vijana kutoka nchi jirani ya Burundi.


"Kwa wale vijana watakaohitaji kufadhiliwa katika jambo hili jema, fomu zitaanza kutolewa kuanzia Aprili 10 hadi Aprili 30. Hivyo, wanakaribishwa kuchukua bila kusita," aliongeza Kishki.


Mbali na udhamini wa ndoa, Shekhe Kishki amesema taasisi hiyo kwa mwaka huu pia itatoa udhamini wa kuwasaidia watu wapatao 1,050 wanaohitaji kutahiriwa.


"Tunatoa huduma hii bure kwa wale wote, iwe ni watoto au watu wazima wanaohitaji kufanyiwa twahara. Gharama zote zitagharamiwa na taasisi yetu," alisema Kishki.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.