Simulizi ya Kutisha Bangkok: Simba Wamrarua Mlinzi Mzoefu Mbele ya Watalii

international | Thu Sep 11 2025


Simulizi ya Kutisha Bangkok: Simba Wamrarua Mlinzi Mzoefu Mbele ya Watalii

Tukio la kutisha na kusikitisha limetokea katika Hifadhi maarufu ya Wanyama ya Safari World jijini Bangkok, nchini Thailand, baada ya mlinzi na mhudumu mzoefu wa wanyama kushambuliwa na kuuawa kikatili na kundi la simba mbele ya kadhaa ya watalii waliokuwa wameshika tama.


Tukio hilo la kutisha, lililotokea juzi mchana, lilimhusisha Jian Langkarasami (58), ambaye alikuwa na uzoefu wa miaka 30 katika kazi hiyo. Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha mlinzi huyo akisimamisha gari lake na kushuka ndani ya eneo la wazi la simba. Ghafla, simba mmoja alimvizia kimyakimya kutoka upande wa nyuma ambao hakuwa akiona, akamrukia na kumwangusha. Mara moja, simba wengine walifuata na kumvamia kwa pamoja, wakimrarua kwa takribani dakika 15.


Watalii waliokuwa ndani ya magari yao ya kitalii walishuhudia tukio zima kwa macho yao wakiwa wamejawa na hofu na mshtuko, bila uwezo wa kutoa msaada wowote. Mmoja wa mashuhuda aliliambia gazeti la nchini humo, "Tulimwona mwanaume akishuka kwenye gari na kusimama peke yake kwa kama dakika tatu, jambo lililotushangaza. Ghafla simba alimrukia kutoka mgongoni, na hata hakupata nafasi ya kupiga kelele."


Inasikitisha zaidi ni kwamba, marehemu alikuwa mtaalamu aliyebobea, akiwa amefanya kazi katika hifadhi hiyo kwa miaka 30, na zaidi ya miaka 20 alikuwa akihudumia wanyama wakali kama simba na chui. Bado haijafahamika wazi kwa nini mtaalamu huyo alichukua uamuzi wa hatari wa kushuka kwenye gari bila vifaa vya kujilinda. Hata hivyo, chombo kimoja cha habari cha nchini humo kilidokeza kuwa huenda alikuwa akiokota kitu kilichomuanguka, na alipoinama kukiokota, ndipo simba walipomshambulia.


Baada ya shambulio hilo, wahudumu wenzake walifanikiwa kumwokoa na kumkimbiza hospitalini, lakini alifariki dunia kutokana na majeraha makubwa shingoni, tumboni na miguuni.


Uongozi wa Safari World umefunga eneo hilo kwa muda na unaendelea na uchunguzi. Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Hifadhi za Taifa na Wanyamapori nchini Thailand, Athapol Charoenchansa, alisema, "Inaonekana shambulio lilitokea wakati simba walipokuwa wakila. Tunadhani simba mmoja hakuwa na hisia nzuri na ndiye aliyeanzisha shambulio."


Safari World ni hifadhi kubwa zaidi ya wanyama jijini Bangkok na huvutia watalii wengi, ambapo hutoa fursa kwa wageni kuona wanyama wakizunguka kwa uhuru. Watalii hulipa takribani Baht 1,200 (kama Shilingi 85,000 za Kitanzania) kwa ajili ya kushiriki katika zoezi la kuwalisha simba na chui.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.