Polisi nchini Costa Rica wamewatia mbaroni watu wanne—wanaume watatu na mwanamke mmoja—kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kinyama ya Roberto Samcam, aliyekuwa Meja wa jeshi la Nicaragua na mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Daniel Ortega. Tukio hili la mauaji limetuma ujumbe wa hofu kwa Wanicaragua wengine wanaoishi uhamishoni kwa kupinga utawala wa Ortega.
Washukiwa hao wanne wanakabiliwa na tuhuma za kupanga na kutekeleza mauaji ya Samcam yaliyotokea mwezi Juni mwaka huu. Inaripotiwa kuwa siku ya tukio, wauaji walijifanya kuwa wasafirishaji wa mizigo au wapangaji wapya ili kuwahadaa walinzi katika lango la eneo la makazi alilokuwa akiishi Samcam. Baada ya kufanikiwa kuingia, walimfuata nyumbani kwake, wakampiga risasi nane na kisha kutoroka kwa kutumia pikipiki. Samcam, mwenye umri wa miaka 66, alifariki papo hapo.
Roberto Samcam alikuwa miongoni mwa sauti zenye ushawishi mkubwa zilizokuwa zikikosoa serikali ya Nicaragua akiwa uhamishoni. Baada ya kustaafu jeshini, aligeuka kuwa mpinzani mkali wa Rais Ortega, hali iliyosababisha mateso kutoka kwa serikali na kumlazimu yeye na mkewe kukimbilia nchi jirani ya Costa Rica mnamo mwaka 2018.
Akiwa uhamishoni, aliendeleza mapambano yake kupitia uandishi wa vitabu na mahojiano na vyombo vya habari, akifichua bila woga maovu na ufisadi ndani ya jeshi la Nicaragua, ambalo anasema linatumiwa na Ortega kulinda utawala wake. Cha kushangaza ni kwamba, Samcam aliuawa siku moja tu baada ya kufanya mahojiano na kituo kimoja cha habari akielezea vitendo vya kiimla na vya kukandamiza demokrasia vinavyofanywa na chama tawala cha FSLN kinachoongozwa na Ortega.
Mnamo Februari 2023, serikali ya Nicaragua ilimvua uraia wake kwa kumtangaza kama "msaliti wa taifa." Kifo chake kimeleta mshtuko mkubwa miongoni mwa raia wa Nicaragua walio uhamishoni, ambao wanamtaja kama mmoja wa wakosoaji imara zaidi wa utawala wa Ortega.
Rais Daniel Ortega amekuwa madarakani nchini Nicaragua kwa vipindi virefu, kuanzia 1985 hadi 1990 na kisha kurejea tena mwaka 2007 hadi sasa. Ameimarisha utawala wake kwa kuwakandamiza vikali wapinzani, hasa wakati wa maandamano makubwa ya mwaka 2018 na uchaguzi mkuu wa 2021. Kimataifa, amekuwa akijenga urafiki wa karibu na nchi kama Korea Kaskazini na China, huku hivi karibuni akifunga ubalozi wake nchini Korea Kusini na kumteua balozi mpya wa Korea Kaskazini. Isitoshe, Ortega alitumia wingi wake bungeni kupitisha mfumo wa kipekee wa "urais wa pamoja," na kisha kumteua mke wake, Rosario Murillo, kuwa rais mwenza bila kupitia uchaguzi.