Kashmir, eneo lenye mandhari ya kupendeza kaskazini mwa India, limetumbukia katika majonzi baada ya mafuriko ya ghafla na maporomoko ya ardhi kusababisha maafa makubwa, yakiacha nyuma vifo na uharibifu. Kulingana na shirika la habari la Reuters, zaidi ya watu 60 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 100 bado hawajulikani waliko, wakihofiwa kuwa wamefunikwa na vifusi.
Janga hili limetokea katika eneo la Choshti, ambapo maji yaliyochanganyika na tope yaliwafagilia mbali mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya chakula cha mchana. Eneo la Choshti lina umuhimu mkubwa wa kiroho, kwani ndio kituo cha mwisho cha barabara kwa mahujaji wanaoenda katika Hekalu la Machail Mata, lililopo katika milima mirefu ya Himalaya.
Waokoaji wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana, wakitumia zana za mikono kama vile majembe na kamba, wakijaribu kuwatafuta manusura waliofukiwa chini ya vifusi. Mamlaka inakadiria kuwa kuna uwezekano wa watu 100 hadi 150 bado wamekwama chini ya vifusi, na juhudi za uokoaji zinaendelea kwa kasi kubwa.
Hali kama hii imekuwa ikitokea mara kwa mara katika milima ya Himalaya, ambapo mafuriko na maporomoko ya ardhi huathiri maeneo mbalimbali. Inasemekana kuwa siku chache zilizopita, yaani Agosti 5, Jimbo la Uttarakhand lilishuhudia janga jingine la mafuriko liloangamiza kijiji kizima na kuua zaidi ya watu 70.
Matukio haya yanaashiria hatari kubwa inayowakabili wakazi na mahujaji katika maeneo haya ya milima, na kusisitiza umuhimu wa Serikali kuchukua hatua madhubuti za kuzuia majanga na kuwajali watu wanaotembelea maeneo hayo. Janga hili limeweka wazi udhaifu wa miundombinu katika maeneo ya mbali na jinsi hali ya hewa inavyoweza kugeuka na kusababisha maafa makubwa kwa ghafla.