Gazeti la Wall Street Journal (WSJ) linaripoti kuwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imethibitisha kuongeza kwa haraka idadi ya wanajeshi wake katika eneo la Mashariki ya Kati.
Rais wa Marekani, Donald Trump, hivi karibuni alitishia kuishambulia Iran ikiwa haitakubali kujadiliana kuhusu kupunguza programu yake ya nyuklia.
Hata hivyo, vyanzo viwili vimedokeza kuwa ongezeko hili la sasa la wanajeshi wa Marekani Mashariki ya Kati linalenga kuimarisha operesheni dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen na kuizuia Iran, na siyo maandalizi ya kushambulia Iran moja kwa moja.
Jeshi la Marekani linaongeza idadi ya ndege zake za kivita za F-35 katika eneo hilo, ambazo zitajiunga na ndege za kivita za B-2 na droni za Predator ambazo tayari ziko Mashariki ya Kati. Aidha, taarifa za ufuatiliaji wa anga zinaonyesha kuongezeka kwa idadi kubwa ya ndege za usafiri na ndege za kujaza mafuta za Jeshi la Wanahewa la Marekani zikielekea Mashariki ya Kati kutoka Ulaya, Asia, na Marekani bara.
Hivi karibuni, vikosi viwili vya manowari vitakuwa vimepelekwa Mashariki ya Kati. Kimoja ni kundi la manowari linaloongozwa na USS Harry S. Truman, ambalo limekuwa katika eneo hilo tangu msimu uliopita wa vuli. Kikosi kingine, kinachoongozwa na USS Carl Vinson, ambacho hapo awali kilikuwa kimepelekwa Asia, kinatarajiwa kuwasili ndani ya wiki mbili.
Vikosi vya manowari kwa kawaida hujumuisha manowari mbalimbali, ikiwa ni pamoja na waharibu waliobeba makombora ya kusafiri kwa umbali mrefu.
Jeshi la Marekani pia linapeleka mifumo ya kujihami ya makombora ya Patriot kwenye kambi zake za Mashariki ya Kati ili kulinda kambi hizo na washirika wake.
Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Houthi kila siku tangu tarehe 15 mwezi uliopita.
Iran imekuwa ikiwapa waasi wa Houthi silaha na mafunzo. Mazungumzo kati ya Marekani na Iran kuhusu programu ya nyuklia ya Iran bado hayajapangwa, na Marekani imeonya kuwa itawajibisha Iran ikiwa waasi wa Houthi watawashambulia wanajeshi wa Marekani.
Iran nayo imeahidi kujibu kwa kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani Mashariki ya Kati ikiwa Marekani itaiandama. Afisa mmoja wa Iran alisema kuwa kambi za Marekani zinazozunguka Ghuba ya Uajemi zitakuwa shabaha ya majibu, akiongeza kuwa "wanajeshi wote wa Marekani watakuwa shabaha."