Marekani: Sherehe ya Wanafunzi wa Zamani Yageuka Mauti, Wanne Wauawa kwa Risasi

international | Mon Oct 13 2025


Marekani: Sherehe ya Wanafunzi wa Zamani Yageuka Mauti, Wanne Wauawa kwa Risasi

Taharuki na simanzi vimetanda katika kisiwa cha St. Helena, jimbo la South Carolina nchini Marekani, kufuatia tukio la kinyama la ufyatuaji wa risasi lililotokea kwenye eneo la burudani na kusababisha vifo vya watu wasiopungua wanne. Mkasa huu, ambao pia umewaacha wengine zaidi ya ishirini na majeraha, ulitokea majira ya saa saba za usiku wa Jumamosi, na kubadilisha shamrashamra za sherehe kuwa eneo la damu na maafa.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya kimataifa, shambulio hilo lilifanyika katika baa moja iliyoko katikati ya jamii ya Gullah, wakati mamia ya watu walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya sherehe ya wahitimu wa zamani wa shule ya sekondari ya Beaufort Battery Creek, iliyoko takriban kilomita 16 kutoka eneo la tukio. Ghafla, mazingira ya furaha yaligeuka kuwa ya hofu kubwa baada ya milio ya risasi kuanza kusikika, na kuwaacha watu wakipambana kuokoa maisha yao.


Mamlaka za usalama katika eneo la Beaufort zimeeleza kuwa mbali na vifo hivyo vinne, wapo majeruhi wengine ishirini, ambapo wanne kati yao wako katika hali mahututi, wakipigania uhai wao hospitalini. Hadi sasa, utambulisho wa waathirika, wakiwemo waliofariki na majeruhi, bado haujawekwa wazi kwa umma. Ofisi ya Sheriff wa Kaunti ya Beaufort imesisitiza kuwa haitatoa majina ya marehemu hadi pale familia zao zitakapokuwa zimejulishwa rasmi, ikiwa ni hatua ya kuheshimu taratibu na faragha za familia zilizoondokewa.


Tukio hili ni mwendelezo wa matukio ya kusikitisha ya unyanyasaji wa kutumia silaha za moto ambayo yameendelea kuwa janga sugu nchini Marekani, na kuacha jamii nyingi katika majonzi na maswali yasiyo na majibu.


The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.