Mafuriko makubwa yameikumba Gaborone, mji mkuu wa Botswana, na kusababisha kufungwa kwa shule na barabara huku maeneo mengi yakiwa chini ya maji.
Rais wa Botswana, Dumo Boko, ametangaza kupitia mtandao wa kijamii kuwa mji mkuu unakabiliwa na athari kubwa za mvua kubwa na mafuriko.
"Leo nimetembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko. Nimeshuhudia uharibifu wa miundombinu na makazi ya watu. Ninatoa pole zangu za dhati kwa wahanga wa janga hili," amesema Rais Boko.
Nyumba na biashara zimeharibiwa vibaya, huku watabiri wa hali ya hewa wakionya kuwa mvua zaidi ya 50mm inaweza kunyesha katika saa 24 zijazo, jambo linaloweza kuongeza athari za mafuriko.
Serikali imetoa tahadhari kuwa maji yanaweza kujaa zaidi katika maeneo ya mabonde, hali inayoweza kuathiri miundombinu na kusababisha hasara zaidi kwa mali za wananchi.