Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ametoa msimamo mkali, akisisitiza kuwa taifa hilo halitapiga goti mbele ya vitisho vya kijeshi kutoka Marekani. Akijibu matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, Donald Trump, Khamenei amesisitiza kuwa uvamizi wowote wa kijeshi utakuwa na matokeo yasiyoweza kurekebishwa.
Shirika la Habari la Iran (IRNA) na Tasnim, yakimnukuu Khamenei katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake kwenye runinga ya taifa Alhamisi, Juni 18, 2025, ziliripoti kuwa kiongozi huyo alisema, “Marekani inapaswa kujua kwamba Iran haitasalimu amri.” Aliongeza kuwa Wairani watasimama kidete dhidi ya “vita vya kulazimishwa na amani ya kulazimishwa,” akisisitiza kuwa "watu hawatajinyenyekeza kwa shinikizo lolote kutoka kwa mtu yeyote."
Khamenei alionya kuwa yeyote anayejua historia ya Iran hatawahi kuzungumza na Wairani kwa lugha ya vitisho, akifafanua kuwa "Wairani si watu wa kusalimu amri." Kauli hii inakuja kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa Donald Trump, ambaye Jumanne, Juni 17, 2025, alichapisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social akitaka "Iran isalimu amri bila masharti." Trump pia alionya kuwa "uvumilivu wetu umekwisha," akidokeza uwezekano wa kushambulia Khamenei mwenyewe.
Vyombo vya habari vya Marekani kama CNN na New York Times vimeripoti kuwa Trump anazidi kuunga mkono matumizi ya mali za Marekani kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran. Hali hii inaongeza wasiwasi wa kuibuka kwa mzozo mpya katika eneo la Mashariki ya Kati, tayari lililojaa mivutano.
Matamshi ya Khamenei yamekuja siku tano tu baada ya hotuba yake ya awali ya Juni 13, ambapo alionya Israel. Hotuba hiyo ilitolewa baada ya Israel kudaiwa kushambulia na kuua makamanda wakuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Katika hotuba yake ya awali, Khamenei alisisitiza kuwa "shambulio hili limeisababishia Israeli hatima chungu," na kwamba watapokea "adhabu kali." Matamshi haya yanaashiria kuwa mivutano kati ya Iran na washirika wake, pamoja na Israel na Marekani, inaendelea kukua na huenda ikachukua mkondo mwingine hatari.
Iran imekuwa ikitekeleza sera ya "upinzani thabiti" dhidi ya vitisho vya Magharibi, hasa vile vinavyohusiana na mpango wake wa nyuklia na ushawishi wake wa kikanda. Serikali ya Iran inaamini kuwa msimamo wao thabiti ndio njia pekee ya kulinda uhuru na maslahi ya taifa lao dhidi ya kile wanachokiona kama ubeberu wa Magharibi. Hali hii ya mivutano inaweza kuwa na athari kubwa kwa bei za mafuta duniani na usalama wa kimataifa kwa ujumla.