Rais wa Kenya, William Ruto, amewashukia vikali wapinzani wake wa kisiasa na wakosoaji wengine, akisema wanajenga taswira hasi isiyo ya kweli kuhusu nchi hiyo. Ametetea kwa nguvu maamuzi yake ya kiuchumi na kusisitiza kuwa serikali yake haitayumbishwa na maneno ya watu aliowaita "wanaotaka kuivuruga nchi."
Akizungumza Jumanne, Rais Ruto alipuuzilia mbali ukosoaji unaoelekezwa kwa serikali yake, akisema Kenya imepiga hatua kubwa za kiuchumi kwa muda mfupi, jambo ambalo nchi nyingi duniani haziwezi kulifanikisha.
"Lazima tuwakatae wale wanaotaka kutuambia kuwa Kenya ni nchi iliyoshindwa. Eti wanazungumza kana kwamba Kenya ndiyo nchi mbaya zaidi duniani. Je, wanajua hata nchi iliyoparaganyika inaonekanaje?" alihoji Rais Ruto kwa ukali.
Alisisitiza kuwa amechukua maamuzi magumu na yasiyokuwa maarufu ili kuleta utulivu katika uchumi wa nchi na wala hajuti kwa hilo. "Unaweza kusema chochote unachotaka. Nimelazimika kufanya maamuzi magumu sana ili kutufikisha hapa na sijutii hata kidogo," aliongeza.
Rais Ruto alisisitiza kuwa ajenda yake ya kupunguza gharama ya maisha, kuimarisha usalama wa chakula, na kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana bado haijabadilika. Alisema serikali yake ina mpango thabiti wa kuendeleza uchumi na kuwaomba Wakenya wasidanganywe na wasiopoitakia mema nchi yao.