Mamlaka nchini Hispania imelazimika kufunga eneo la pwani maarufu la kitalii la Costa Blanca lenye urefu wa kilomita 11, baada ya kuonekana kwa kiumbe kidogo cha baharini chenye sumu kali kinachofahamika kwa jina la "Blue Dragon" au Joka la Bluu. Licha ya urembo wake wa kuvutia, kiumbe hiki kinasifika kwa kuwa "muuaji mrembo zaidi baharini" kutokana na sumu yake inayoweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu.
Tahadhari ya juu imetolewa na serikali za mitaa, huku meya wa eneo la Guardamar del Segura, Bwana José Luis Sáez, akithibitisha kupitia mitandao ya kijamii kwamba viumbe hawa wawili wameonekana ufukweni. Alionya umma vikali akisema, "Ingawa wana rangi za kuvutia na ukubwa mdogo wa takriban sentimita 4, wana sumu kali. Msisogelee wala kuwagusa kwa hali yoyote."
Uwezo wa Joka la Bluu unatokana na tabia yake ya kula seli za sumu kutoka kwa kiumbe kingine hatari sana cha baharini kijulikanacho kama 'Portuguese man o' war'. Baada ya kula, huhifadhi na kuitumia sumu hiyo mwilini mwake, na kuifanya iwe na ukali zaidi kuliko ile ya kiumbe alichokila. Cha kushangaza zaidi ni kwamba, kiumbe hiki hakisiti hata kula wenzake wa aina yake.
Madhara ya kugusana na Joka la Bluu yanaweza kuwa makubwa. Mtu akidungwa, sumu iliyohifadhiwa huingia mwilini na kusababisha dalili kama kichefuchefu, maumivu makali, na kutapika. Ingawa mara nyingi si hatari ya kuua, inaweza kusababisha mzio mkali na hata kifo kwa watu walio katika makundi hatarishi kama watoto, watu wenye mzio, au wale wenye matatizo ya moyo na mfumo wa upumuaji. Hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo mtu atadungwa mara kadhaa.
Kutokana na tishio hili, mamlaka za mji zimeanzisha doria baharini ili kufuatilia iwapo kuna viumbe wengine wanaosukumwa na mikondo ya maji kuelekea fukweni. Wananchi wametakiwa kutoa taarifa haraka kwa waokoaji au mamlaka husika pindi wanapomwona kiumbe huyo. Aidha, wametoa ushauri kwamba endapo mtu atadungwa, anapaswa kuosha eneo lililoathirika kwa maji ya bahari na kwenda haraka kwenye kituo cha huduma ya kwanza au hospitali.
Hii si mara ya kwanza kwa tukio la aina hii kutokea. Mwaka 2018, mvulana wa miaka 11 alikimbizwa hospitalini baada ya kudungwa, hali iliyosababisha kufungwa kwa eneo la pwani lenye urefu wa kilomita 120, ikionyesha uzito wa tishio linaloletwa na kiumbe huyu mdogo lakini hatari.