Hali ya hewa nchini Iran imebadilika ghafla na kuwa ya 'joto kali' la kisiasa na kiuchumi. Wakati Watanzania tukiendelea kuchapa kazi kujenga taifa, huko Mashariki ya Kati, hususan katika mitaa ya Tehran, mambo ni "kulia na kusaga meno." Wimbi kubwa la maandamano limeikumba nchi hiyo huku wananchi wenye hasira wakiingia barabarani kupinga kile wanachokiita kushindwa kwa serikali kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha na kuporomoka kwa thamani ya pesa yao.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotua kwenye dawati la habari kutoka vyanzo vya kimataifa ikiwemo New York Times, maandamano haya sio ya kawaida. Picha na video zinazosambaa kwa kasi mitandaoni zinaonyesha askari wa kutuliza ghasia wakilazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya umati wa watu waliochoshwa na hali ngumu. Hii ni baada ya wananchi kuona "maji yamezidi unga" na kuamua kupaza sauti zao hadharani.
Kiini cha mgogoro huu ni uchumi ulioyumba vibaya. Takwimu zinaogofya; mfumuko wa bei umepaa na kufikia zaidi ya asilimia 42.2 kwa mwaka. Hii ina maana gani kwa mtu wa kawaida? Ina maana bidhaa uliyokuwa ukinunua kwa Shilingi 10,000 sasa inakaribia Shilingi 15,000 au zaidi ndani ya muda mfupi.
Kilio kikubwa zaidi kipo kwenye mifuko ya wafanyakazi. Thamani ya mshahara wa mfanyakazi wa Iran imepigwa na dhoruba kali. Mfanyakazi mmoja jijini Tehran amekaririwa akisema kuwa ndani ya miezi miwili tu, uwezo wa mshahara wake kufanya manunuzi (purchasing power) umeshuka kutoka Dola 300 (sawa na takriban Shilingi za Kitanzania 800,000) hadi kufikia Dola 200 (sawa na takriban Shilingi 530,000).
"Hali ni mbaya, mshahara wangu sasa hautoshi hata kulipia theluthi mbili ya mahitaji ya mwezi. Tumeacha kula nyama, na mambo ya kupeleka gari gereji au kugharamia matibabu ya wazazi yamebaki kuwa ndoto," alilalamika mwananchi huyo kwa uchungu, akigusia uhalisia ambao hata hapa nyumbani tunaufahamu kama 'ukata'.
Kutokana na shinikizo hili, "kichwa" cha kwanza kimekatwa serikalini; Gavana wa Benki Kuu ya Iran, Mohammad Reza Farzin, ametangaza kujiuzulu, ishara tosha kuwa mambo yamemshinda.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amekiri kuwa hali ni tete. Katika hotuba yake bungeni ambayo ilijaa unyenyekevu na lawama kwa watangulizi wake, Rais huyo alisema serikali inatamani kupandisha mishahara lakini hazina haina uwezo huo. Kama ilivyo desturi ya wanasiasa wengi duniani wanapobanwa, alitupa mpira kwa serikali iliyopita na Bunge, akidai kuwa sera mbovu za huko nyuma ndizo zimefikisha nchi hapo ilipo.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanataja sababu kuu tatu za anguko hili: Kwanza ni usimamizi mbovu wa uchumi wa ndani. Pili ni gharama kubwa za vita, ambapo serikali ililazimika kutumia fedha nyingi za benki za ndani kufadhili mzozo wake na Israel mwezi Juni mwaka huu. Tatu, ni "pini" zilizokazwa na Marekani, hususan vikwazo vya mafuta vilivyosimamiwa kidete na utawala wa Donald Trump, ambavyo vimeibana Iran pumzi katika soko la kimataifa.
Hali inaonekana kuwa ngumu zaidi mbeleni baada ya Bunge la nchi hiyo kukataa kupitisha bajeti ya mwaka 2026 iliyopendekezwa na serikali, ambayo ililenga kuongeza kodi na kupunguza matumizi ili kuziba pengo la mapato ya mafuta. Kwa sasa, Iran ipo njia panda, na wananchi wanasubiri kuona nani atakuwa mkombozi wao katika janga hili la kiuchumi.